Timu zitakavyokuwa bize kusajili mastaa Januari hii
Muktasari:
- Dirisha la majira ya baridi huko nyuma limekuwa na utulivu sana, lakini mwaka huu mambo yanaonekana yatakuwa tofauti. Manchester United ipo kwenye uhitaji mkubwa wa kuboresha kikosi chake baada ya kufanya hovyo kwenye Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: DIRISHA la Januari 2025 la usajili wa mastaa wa soka limefunguliwa - na bila shaka klabu zitakwenda kuwa bize kwelikweli kusaka wakali wapya.
Dirisha la majira ya baridi huko nyuma limekuwa na utulivu sana, lakini mwaka huu mambo yanaonekana yatakuwa tofauti. Manchester United ipo kwenye uhitaji mkubwa wa kuboresha kikosi chake baada ya kufanya hovyo kwenye Ligi Kuu England.
Miamba hiyo ya Old Trafford imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumsajili Viktor Gyokeres na Randal Kolo Muani. Kuna mastaa wao pia huenda wakafunguliwa mlango wa kutokea, akiwamo Marcus Rashford na Joshua Zirkzee, ambao maisha yao yana shaka kubwa ya kuendelea kubaki Man United.
Vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool nao wana kitu cha kufanya kwenye dirisha hili. Mohamed Salah na Virgil van Dijk wanaweza kuingia kwenye mazungumzo na klabu za ng’ambo kwa ajili ya kusaini dili za awali. Real Madrid ilishatuma maombi huko Anfield kwa ajili ya kumsajili Trent Alexander-Arnold.
Huko kwingineko, Manchester City, Chelsea na Arsenal - sambamba na timu nyingine kwenye Ligi Kuu England zitakuwa bize kwenye dirisha hili kujaribu kutafuta namna bora ya kuboresha vikosi vyao. Kuna dili kadhaa zinatazamiwa kutokea katika usajili wa dirisha hili la Januari 2025.
Staa wa Frankfurt, Omar Marmoush ameripotiwa kuwa kwenye mazungumzo na klabu ya Arsenal. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri, ambaye amefunga mabao 13 na asisti saba katika mechi 15 alizocheza kwenye Bundesliga, amekuwa akihusishwa pia na klabu za Liverpool na Man City.
Hata hivyo, mwenyewe alisema: “Ninachoweza kuwaahidi mashabiki nitaendelea kujitolea kwa nguvu zote hapa Eintracht. Sifikirii kuhama. Ninaishi hapa na ninafurahia nyakati zangu za kuwapo Frankfurt.”
Huko Anfield kinachoelezwa ni kwamba Van Dijk na Salah wanakaribia kusaini dili jipya, lakini Trent Alexander-Arnold anaweza kuachana na timu hiyo kwenye dirisha la Januari ili asiondoke bure mwisho wa msimu. Ripoti zinafichua Van Dijk na Salah kuna uwezekano mkubwa wa kusaini mikataba mipya Anfield.
Lakini, kwenye kambi hiyo hiyo ya Liverpool, kuna staa mwingine ambaye anaweza kuonyeshwa mlango wa kutokea, ambaye ni Darwin Nunez. Na kama staa huyo wa Uruguay ataondoka, basi kocha wa Liverpool, Arne Slot anaweka nguvu kwenye kumnasa staa wa Inter Milan, Marcus Thuram na straika wa Newcastle United, Alexander Isak.
Kuhusu Man United, ukiwaweka kando Gyokeres na Kolo Muani, miamba hiyo ya Old Trafford imeripotiwa kuwa na mpango wa kunasa saini ya kiungo mshambuliaji wa Barcelona, Dani Olmo, licha ya wakala wa mchezaji huyo kudai kwamba huenda ishu ya mchezaji huyo kuondoka dirisha hili ikawa ngumu.
Hatima ya Olmo kwenye kikosi cha Barcelona ipo kwenye wasiwasi mkubwa kutokana na klabu hiyo ya Catalunya kukabiliwa na ukata.
Lakini, wakala wa mchezaji huyo alisema mchezaji wake hawezi kuhama kwenye dirisha hili na hawakaribishi ofa yoyote. Ukiwaweka kando Man United wanaomtaka Olmo, Liverpool nao wameripotiwa kwenye mchakamchaka wa kutaka saini ya kiungo huyo wa zamani wa RB Leipzig.
Man United inaweza kuachana na Zirkzee hasa baada ya Juventus kuonyesha dhamira ya kuhitaji huduma ya Mdachi huyo, wakitaka akaungane na kocha Thiago Motta, ambaye walikuwa pamoja pia Bologna.
Kwa ujumla wake, kwenye Ligi Kuu England karibu kila klabu itaingia sokoni kunasa walau mchezaji mmoja kwenye dirisha hili la Januari, kuanzia kwa Liverpool, Man United, Tottenham, Southampton, Man City, Arsenal na Leicester City kwa kuzitaja kwa uchache. Na kitu kizuri kwenye ligi hiyo, kuna wachezaji 82, ambao mikataba yao itafika tamati mwishoni mwa msimu huu akiwamo Mo Salah, Jamie Vardy, Harry Maguire na wengineo.