Simbu: Maajabu yalianza hapa!
Muktasari:
- Safari yake ni ya kuvutia kutoka mashindano ya mtaa na mazoezi ya chini ya joto la Singida hadi podium ya dunia, Simbu amejenga historia isiyosahaulika kwa Tanzania.
KILA Taifa lina nyota wake, na Tanzania sasa inajivunia mmoja wa wandaaji wa historia ya riadha duniani ambaye ni Alphonce Simbu, kutoka kijiji cha Mampando wilayani Ikungi, Singida, situ ni mwanariadha, bali ni alama ya bidii isiyo na kifani, uvumilivu na nidhamu isiyokoma.
Safari yake ni ya kuvutia kutoka mashindano ya mtaa na mazoezi ya chini ya joto la Singida hadi podium ya dunia, Simbu amejenga historia isiyosahaulika kwa Tanzania.
Hadi Alphonce kuanza kushiriki kikamilifu, Tanzania ilikuwa na medali moja pekee kwenye historia yake ya mashindano ya dunia tangu ilipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1983 Helsinki Finland ikiwakilishwa na baadhi ya nyota akiwemo Gidamis Shahanga, Zakaria Barie na Abraham Mikumi.
Medali ya kwanza kupatikana ikawa ni ya fedha kupitia kwa Christopher Isengwe mwaka 2005 baada ya kufanya kazi iliyowashinda wengi kwa miaka 22, hapo hapo Helsinki, Finland akamliza wa pili kwa muda wa saa 2:10:21, ndie alianza kuandika rekodi mpya kwa Tanzania.
Baada ya miaka 13 kupita Tanzania ikapata medali ya pili, lakini mara hiyo ikawa ya shaba kupitia kwa Alphonce aliyemaliza wa tatu kwenye mashindano hayo ya dunia mwaka 2017, London Uingereza kwa muda wa saa 2:09:51, zikawa ndio medali za kutamba nayo huku medali ya dhahabu ikawa ndoto isiyotimika.
Septemba 15, 2025 rekodi mpya ikawekwa baada ya kupita miaka 42 tangu Tanzania ilipoanza kushiriki mashindano ya dunia bila kuambulia medali ya dhahabu, mara hii akawa ni yule yule kijana kutoka Mampando, Sajenti Alphonce Felix Simbu, mwanariadha wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ndie aliyeweka rekodi ambayo haiwezi kusahaulika.
Akiwa katika jiji la Tokyo, Japan aliwashangaza wengi kwa kuwashinda wababe ambao walipewa nafasi, Simbu akiwa katika kiwango bora alimaliza wa kwanza mbio ndefu upande wa Wanaume kwa muda wa saa 2:09:48, akifuatiwa na Mjerumani Amanal Petros ambaye alimaliza nae muda sawa, Simbu akitanguliza mguu wa kwanza.
Mwanaspoti imekuchambulia sababu ambazo zimepelekea Simbu kushinda mbio na kuweka rekodi mpya ya Tanzania kupata medali ya kwanza ya dhahabu katika mashindano hayo.
Kuongezeka kwa kiwango
Akiwa na umri wa miaka 24, 2016 alionyesha kiwango chake kilichoanza kuongezeka mara kwa mara, mbio zake za mwanzo zilikuwa alama ya kuonyesha jitihada zake na uwezo wa kuvumilia majaribu.
Mwaka huo aliwakumbusha Watanzania kwamba hakuna njia ya mkato katika riadha kwani aliweza kumaliza nafasi ya tano katika marathoni za Olimpiki za Rio de Janeiro, Brazil, kwa kutumia muda wa 2:11:15.
Njia yake ya kuonyesha kwamba bidii pekee ndiyo ufunguo wa mafanikio iliwavunja moyo wale waliokata tamaa, situ wanamichezo bali hata raia wa kawaida, ingawa hakuweza kutwaa medali, aliunda Imani mpya ndani ya taifa kwamba siku moja Tanzania itashinda medali ya dhahabu.
Kiwango chake kilizidi kuongezeka mwaka 2017 pale alipofanikisha kutwaa medali ya shaba kwenye mashindano ya dunia yaliyofanyika London, Uingereza, akitumia muda wa 2:09:51.
Aliendelea kuingia katika nane bora katika Olmpiki mara mbili mfululizo mwaka 2016, Rio de Janeiro Brazil na mwaka 2020 Tokyo Japan akimaliza wa saba kwa muda wa 2:11:35.
Mwaka 2022, juhudi zake zililipwa na medali ya fedha kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyoandaliwa Birmingham, Uingereza, kabla ya mwaka jana 2024 kuweka rekodi yake binafsi ya muda wa 2:04:38 kupitia mbio za Valencia Marathon za nchini Hispania.
Mwaka huu alionyesha nguvu zake za ushindani kwa kumaliza wa pili Boston Marathon kwa muda wa saa 2:05:04 nchini Marekani na kidogo ashinde, hivyo alikuwa anaongeza kiwango kizuri na uimarishaji wa muda ambao anaweza kushindana na mtu yeyote duniani kwa levo ya mashindano ya kimataifa, ambapo kuboreka kwa kiwango chake haikuwa kwa bahati mbaya, bali matokeo ya jitihada endelevu.
Uhalisia wa Mazoezi
Kwa muda wote, Alphonce Simbu alikuwa akifanya mazoezi yake Arusha, jiji lililo na faida kubwa kwa wanariadha wa marathoni, mazoezi haya yalikuwa na faida kuu mbili kubwa anaposhindana kwenye mashindano makubwa kama Tokyo.
Faida ya kwanza ni altitude ya juu ya Arusha, kufanya mazoezi kwenye eneo lenye uwanda wa juu kunasababisha oksijeni kuwa chache hewani, jambo linaloongeza uwezo wa mwili kutumia oksijeni vizuri zaidi.
Hivyo, mwili unapoenda kushindana kwenye eneo la kiwango cha chini cha bahari (sea level) lenye oksijeni nyingi, unapata faida kubwa ya oksijeni, ikimsaidia kustamina, kudumisha kasi, na kudhibiti uchovu kwa ufanisi.
Alphonce alifanya mazoezi kwenye eneo hili la juu kwa muda mrefu, hivyo alipofika Tokyo, alikaa siku chache tu kabla ya mbio kuanza, kwa hivyo hakupoteza nguvu kutokana na tofauti ya joto au hali ya hewa, na aliingia kwenye mashindano akiwa bado kwenye fomu bora, ile ile aliyokuwa nayo wakati wa mazoezi katika viwanja vya Ilboru.
Nia na mzigo wa ushindi.
Alikabidhiwa mzigo mkubwa, kutimiza matarajio ya taifa, alikuwa na nia ya dhahabu kwa Tanzania mara wa mara, akijua kuwa wengi walijaribu bila mafanikio, kauli yake kubwa, “Nina hamu kubwa ya kushinda,” ilichangia motisha ya kushirikiana na wadau wa riadha, Shirikisho la Riadha, wachezajaji wenzake, na mashabiki wa riadha, hivyo aliingia Tokyo akiwa emebeba matumaini ya Watanzania.
Nidhamu
Nidhambu ya sajenti Simbu ilikuwa mojawapo ya siri za mafanikio yake, aliweka ratiba thabiti ya mazoezi, kulala kwa wakati unaofaa, na lishe bora, alijua kuwa ushindi haupatikani bila uvumilivu na utulivu wa akili.
Nidhamu hii ilimsaidia kudumisha hali ya juu ya fomu ya mwili na akili, jambo muhimu hasa katika mashindano makubwa yenye ushindani cha juu.
Programu za Mazoezi
Mbali na nidhamu, Alphonce alipatiwa programu na waalimu wake wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiongozwa na kocha mteule daraja la pili, Antony Mwingereza, programu hii ilibuniwa mahsusi kwa ajili ya marathoni, ikijumuisha mbinu za kuimarisha kasi, uvumilivu, ili kumsaidia kudumisha kiwango cha juu na kumletea ushindi mkubwa, ikithibitisha kuwa mpango mzuri wa mazoezi unachangia sana matokeo ya kimataifa.
Malezi na Usimamizi jeshini
Malezi mazuri na utunzaji wa wanariadha huyo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yalichangia sana mafanikio yake kwani, Jeshi limemsaidia kimaadili, na kiakili, likimfundisha maadili ya nidhamu, uvumilivu, na mshikamano.
Pia alipatiwa usaidizi wa kiutendaji ikiwa ni pamoja na ruhusa za kushiriki mashindano ya kimataifa kwa wakati unaofaa, jambo lililo hakikisha hakuwa na vizuizi vya kisheria au kiutendaji akishiriki vyema mashindano mengi ikiwemo yale ya mwaka jana kwa maana ya mbio za Valencia, mwaka huu Boston na kuweka rekodi ambayo ilisubiriwa kwa hamu nchini ya kupata medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia.
Utunzaji huu wa kikamilifu ulimsaidia Alphonce kuzingatia mazoezi yake bila wasiwasi huku akitanguliza uzalendo mbele na shauku ya kuiletea taifa heshima.