Serena, Venus kukipiga pamoja Wimbledon
Muktasari:
- Wildcard ni ruhusa maalumu inayotolewa na waandaaji wa mashindano kwa mchezaji kushiriki kwenye mashindano bila kulazimika kufuzu kwa njia za kawaida za viwango vya ubora au mechi za mchujo.
WIMBLEDON,ENGLAND: MASTAA wa tenisi wakongwe, Serena na Venus Williams watafufua ushirikiano wao wa kihistoria katika mechi ya wachezaji wawili wawil, kwenye michuano ya Wimbledon, mwezi huu, baada ya kupewa ‘wildcard’ ya kushiriki kwenye droo ya wanawake ya michuano hiyo.
Wildcard ni ruhusa maalumu inayotolewa na waandaaji wa mashindano kwa mchezaji kushiriki kwenye mashindano bila kulazimika kufuzu kwa njia za kawaida za viwango vya ubora au mechi za mchujo.
All England Club ilitangaza majina ya waliopata wildcard jana Jumanne asubuhi, katika moja ya matangazo yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu kubwa miaka ya karibuni kutokana na kurejea kwa Serena kwenye tenisi ya kulipwa mwezi huu baada ya miaka minne ya kustaafu.
Serena, bingwa mara saba wa mchezo wa mmoja mmoja hakuomba wildcard ya kushiriki mchezo wa mmoja mmoja katika michuano hiyo na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 44 ameendelea kuwa na msimamo wa kutotoa majibu ya wazi anapoulizwa kama ana mpango wa kurejea katika mchezo wa mmoja mmoja.
Venus, bingwa mara tano wa mchezo wa mmoja mmoja pia hajapewa wildcard ya mchezo wa mmoja mmoja, lakini ameendelea kushiriki mashindano tangu alipoanza taaluma yake 1994, akisimama tu kutokana na changamoto za kiafya. Anatimiza umri wa miaka 46, leo, Jumatano.
Kamati ya wildcard ya Wimbledon pia ilikuwa na uamuzi mgumu zaidi wa kufanya mwaka huu, ambapo Maja Chwalinska, mchezaji wa Poland ambaye aliushangaza ulimwengu wa tenisi mwezi huu kwa kufika fainali ya wanawake ya French Open akiwa ametokea hatua za kufuzu pia amepata wildcard.
Licha ya kutokidhi nafasi za viwango vya ubora kwa Wimbledon kutokana na tarehe ya mwisho ya kukata majina kabla ya French Open, Chwalinska atakuwa mmoja wa wachezaji wachache kuwa na hadhi ya wildcard na pia kuwa mchezaji aliyepangwa kwenye mashindano ya Grand Slam kutokana na kupanda kwake kwa kasi katika viwango vya ubora. Kwa sasa anashika nafasi ya 21 duniani.
Pia wametoa wildcard za mchezo wa mmoja mmoja kwa wachezaji wakongwe Stan Wawrinka, ambaye atastaafu mwaka huu, na Grigor Dimitrov. Dan Evans wa Uingereza, ambaye pia atastaafu baada ya michuano hiyo hayupo kwenye orodha ya awali ya mchezo wa mmoja mmoja lakini amepewa wildcard ya mchezo wa wawili pamoja na mwenzake wa Uingereza Henry Searle.
Serena na Venusi ni miongoni mwa jozi zilizofanikiwa zaidi katika historia ya mchezo wa wawili, wameshinda mataji 14 ya Grand Slam pamoja, idadi inayoshika nafasi ya pili kwa ubora katika enzi ya Open kati ya timu zote, na mataji sita ya wanawake ya Wimbledon idadi kubwa zaidi.
Pia wameshinda medali tatu za dhahabu za Olimpiki katika mchezo wa wawili wa wanawake na kufikia nafasi ya kwanza katika viwango vya WTA.