Said Bwanga: Miaka minne bila kipigo, sasa auwinda ubingwa wa Dunia
Muktasari:
- Bwanga alimshinda Chino kwa pointi katika pambano ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki na wapenda masumbwi.
WIKIENDI iliyopita ilichafuka ujumbe mitandaoni wa kumpongeza bondia Said Bwanga mitandaoni baada ya kushinda taji la dhidi ya Said Chino kwenye usiku wa NIGHT 2 REMEMBER pambano la raundi 10 lililopigwa Oktoba 31, 2026 kwenye ukumbi wa The Sky Wave Hall, Kawe.
Bwanga alimshinda Chino kwa pointi katika pambano ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki na wapenda masumbwi.
Haikuwa tu kumpa pongezi baada ya ushindi wake bali pia baadhi ya wadau na mashabiki walimtabiria atakuja kuwa bondia mzuri miaka ijayo kutokana na nidhamu yake.
Na Mwanaspoti limemtafuta na kufanya mahojiano na bondia huyo ambaye anaamini kwake nidhamu ina asilimia kubwa kwa bondia kuliko mazoezi.
NIDHAMU MUHIMU
Bwanga anasema nidhamu ndiyo msingi mkuu unaomfanya mchezo wowote wa ngumi uwe na maana ya kweli, huku akisisitiza kuwa bila nidhamu ya nje na ndani ya ulingo, uwezo wa kiufundi unakuwa hauna kazi.
Anasema mabondia wengi wamekuwa wakileweshwa na sifa za muda mfupi mara baada ya kupata ushindi kwenye mapambano machache, jambo linalowafanya waanze kuwadharau wapinzani wao au kupunguza juhudi kwenye mazoezi.
“Unapomdogosha mpinzani wako au kuacha kuheshimu mchezo, ulingo huwa unakufundisha adabu kwa njia mbaya sana. Kila mara ninapoingia ulingoni, ninajua kabisa kwamba mbele yangu yupo mpinzani aliyefanya maandalizi pia, hivyo lazima nimpe heshima yake inayostahili,” anaongeza Bwanga.
KIPIGO TANGU 2022
Tangu mwaka 2022 bondia huyo hajawahi kupoteza pambano. Akiwa na matokeo mfululizo, Bwanga ameendelea kuwa mwamba asiyetikisika ulingoni, akipata ushindi kwenye mapambano yake yote aliyopigana kuanzia mwaka 2022, 2023, 2024, 2025 hadi kufikia mwaka huu wa 2026 bila kuonja kipigo.
Bwanga anasema “nadhani ni kujifunza ulipokosea kama sijapoteza miaka minne sasa ni wazi kwamba napaswa kuendeleza hilo na kupambana kuhakikisha naendeleza rekodi hiyo.”
Anafafanua kuwa siri kubwa ya kulinda rekodi hiyo isiyo na doa siyo tu kuwa na nguvu za kupigana ulingoni, bali ni uwezo wa kutathmini kila pambano lililopita na kurekebisha makosa madogo madogo yaliyojitokeza.
“Hakuna bondia aliyekamilika. Kila baada ya pambano, hata kama nimeshinda kwa KO au kwa pointi, ninakaa chini na benchi langu la ufundi kutazama picha za pambano na kubaini wapi nilipokosea ili tukaimarishe kwenye mazoezi yanayofuata. Hiyo ndiyo inayonifanya nionekane mpya kila mara ninaporejea ulingoni,” anasema.
MAZOEZI NA LISHE
Mbali na nidhamu na kujifunza, Bwanga anataja ratiba yake ya mazoezi na mlo kama nguzo nyingine muhimu inayomwezesha kuhimili raundi zote 10 bila kuchoka. Anasema mazoezi ya ngumi yanahitaji kujitoa kwa kiwango cha juu na kutokusubiri hadi pambano litangazwe ndipo uanze kujipanga.
“Mimi ni bondia wa muda wote. Hata kama sina pambano lililothibitishwa, ninahakikisha mwili wangu upo kwenye viwango vya ushindani. Hiyo inarahisisha kazi pale promota anapokuja na mkataba wa pambano,” anasema.
Anajiwekea malengo ya kufanya mazoezi mara mbili kwa siku, akizingatia mazoezi ya stamina, mbio, na kuongeza kasi ya ngumi, huku akipokea miongozo mizuri kutoka kwa kocha wake.
WITO KWA CHIPUKIZI
Akiwahimiza mabondia wanaochipukia nchini wanaotamani kufikia mafanikio kwenye mchezo huo, Bwanga anawataka kuweka mbele kazi na kuachana na tabia za kutafuta kiki au sifa za haraka kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuthibitisha uwezo wao ulingoni.
“Mchezo wa ngumi unalipa na una fursa nyingi sana kwa sasa hapa nchini, lakini fursa hizo zitakuja tu kama unajielewa. Baki kwenye msingi wa kazi, fanya mazoezi kwa bidii, na mkabidhi Mungu mipango yako,” anashauri Bwanga.
Ushindi wake dhidi ya Said Chino katika Night 2 Remember umemfanya bondia huyo kuzidi kupanda kwenye viwango vya ubora nchini na kanda ya Afrika Mashariki, huku macho ya wadau wengi wa ngumi za kulipwa yakielekezwa kwake kuona akipiga hatua zaidi kimataifa.
“Bado sijafika natamani kuwa Bingwa wa Dunia, lakini kufika huko kunahitaji uwekezaji sana naamini kama nitawekezewa pesa nina nafasi ya kufanya vizuri kimataifa”.
ANAUTAKA UBINGWA
Bwanga anasema amekuwa na wakati mzuri akicheza na mabondia wa nje lakini kiu yake siku moja alete ubingwa wa Dunia ambao kama atakuwa na mwendelezo huo anaweza kufikia.
“Umekuwa ni mwendelezo bora sana kwangu kwenye kila pambano langu la nje, yaani pambano ninalocheza na mgeni, kuweza kupata matokeo ya mapema sana. Yote hayo ni kwa neema ya aliyetuumba, nidhamu na juhudi,” anasema bondia huyo.
“Pambano dhidi ya Kimario nilimpiga kwa TKO raundi ya pili, Vs Gupreet TKO raundi ya pili, Vs Musuza Hassam TKO raundi ya kwanza unaweza kuniita ‘Champion’ kwa sasa na nitalipokea. Huu ni mwanzo wa kuweza kuweka historia na kwenda kuwa bingwa wa dunia kwa mara ya kwanza, Inshaallah.”