PUMZI YA MOTO: Kama inawezekana kwenye muziki, kwanini ishindikane kwenye mpira
Muktasari:
- Wakati ule Ligi Kuu Tanzania ilikuwa moja, ikiitwa Ligi Kuu ya Muungano (Union Super League), timu za Bara na Zanzibar zilikutana kila mwaka na vumbi lilitimka hasa.
Miaka ya 1980 na hata nusu ya kwanza ya miaka ya 1990 hakukuwa na tofauti kubwa ya nguvu za kiuchumi na ufundi kati ya soka la Bara na Zanzibar.
Wakati ule Ligi Kuu Tanzania ilikuwa moja, ikiitwa Ligi Kuu ya Muungano (Union Super League), timu za Bara na Zanzibar zilikutana kila mwaka na vumbi lilitimka hasa.
Hii ndiyo ilikuwa ligi rasmi ya Tanzania inayotambuliwa na CAF na Fifa na bingwa wake ndiyo alikwenda kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika. Timu za Zanzibar kama Malindi, Miembeni, Small Simba, KMKM na hata Kikwajuni zilikuwa maarufu sana kwa kucheza soka safi na kushindana hasa na timu za Bara.
Haikushangaza KMKM kuwa mabingwa mwaka 1984, Malindi 1988 na 1992. Na hata kimataifa, haikushangaza pia Malindi kufika nusu finali ya Kombe la CAF 1995 na kutolewa kwa penalti na Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani.
Malindi iliundwa na wachezaji nyota kama Edibily Lunyamila, Victor Bambo na Riffat Said kutoka Yanga. Pia nyota wa Zambia aliyecheza fainali ya Afcon 1994, Mordon Malitoli ambaye pia 1990 alicheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika akiwa na Nkana FC.
Pia alikuwepo Julian Albertov, nyota kutoka Bulgaria na kuifanya Malindi kutisha hasa. Kulikuwa na mashindano yaliyoitwa Kombe la Hedex, Malindi waliifunga Simba 5-0 katika Uwanja wa Amaan Zanzibar. Timu za Zanzibar ziliweza kuvuka maji hadi Bara na kuchukua wachezaji tegemeo.
Lakini tofauti ya soka la Zanzibar na Bara kimapato ilianza 1997 pale ligi ya Bara ilipopata mdhamini wa kwanza wa maana. Ulikuwa udhamini kutoka kampuni ya moja ya bia na hata ligi ikaitwa jina la bia hiyo.
Hapo ndipo tofauti ilipoanza. Ligi ya Bara kwa ujumla ilianza kuimarika na kuiacha kidogo kidogo ile ya Zanzibar.
Kwa miaka kadhaa walitokea wadhamini wa vilevi kwa ligi ya Zanzibar, lakini walikataliwa kutokana na utamaduni wao.
Zanzibar hawaruhusu kampuni za vilevi wala kamari kutangaza biashara zao kule. Lakini sasa kuna jambo linakwenda kutokea. Tuzo kubwa za muziki za TRACE zitafanyika Zanzibar mwaka huu kwenye Hoteli ya Mora Resort kuanzia Februari 24 hadi 26.
Wadhamini wakuu wa tuzo hizo ni bia. Kwa hiyo kama kilevi kimeruhusiwa kudhamini tuzo za muziki Zanzibar, kwanini kampuni za wadhamini kama hawa wanazuiwa kwenye mpira. Kama hoja ni maadili, basi hata watu wa muziki pia wakatazwe kudhaminiwa na vilevi isiwe mpira peke yake.
Mbaya zaidi timu za Bara kama Yanga na Simba ambazo hudhaminiwa na kampuni za kamari zinakwenda kuchezea kule na kuvaa jezi zenye matangazo yanayokatazwa. Kama ni maadili, hata Yanga Simba walitakiwa waambiwe kwamba "huku hatutangazi hizo vitu" ili wajue cha kufanya.
Lakini kitendo cha kuzizuia timu Zanzibar na ligi kwa ujumla kudhaminiwa na kampuni kama hiyo huku ni kuendelea kulikwamisha soka la Visiwani. Kampuni za vilevi na kamari ndizo marafiki wakubwa wa soka. Zanzibar iruhusu timu na ligi yao kudhaminiwa na kampuni hizo kwa sababu kwa asilimia kubwa wateja wao ndiyo wako huko.
Ni hadi serikali ya Zanzibar itakapouangalia mpira kwa jicho lile lile kama la Chato, ndio mpira utaanza kurudi zama zile na Malindi kufika nusu fanali ya mashindano ya Afrika.