Namna ya kutathimini uzito uliokithiri
Muktasari:
- Njia hii hujulikana kama kikokotozi cha uwiano wa urefu na uzito wa mwili. Zao linalopatikana linaweza kutoa picha halisi ya hali ya uzito wa mchezaji au mtoto yeyote yule, na hatimaye hatua za kukabiliana na hali hiyo zikachukuliwa.
WIKI iliyopita tuliona tatizo la uzito mkubwa au uzito uliokithiri kwa wanasoka. Leo tutaona njia rahisi ambayo wataalamu wa tiba wanaitumia kutathmini hali ya uzito wa mwili.
Njia hii hujulikana kama kikokotozi cha uwiano wa urefu na uzito wa mwili. Zao linalopatikana linaweza kutoa picha halisi ya hali ya uzito wa mchezaji au mtoto yeyote yule, na hatimaye hatua za kukabiliana na hali hiyo zikachukuliwa.
Katika hali iliyo rahisi, maumbile ya mwanadamu kutokana na uzito yanaweza kuainishwa kama uzito wa chini, uzito wa kawaida, uzito uliozidi, unene na unene uliokithiri.
Mfano, katika shule za soka, huwa ni muhimu sana kujua hali ya uzito ya wachezaji makinda. Hii ni kwa sababu miili yao bado inakua na vilevile miili yao ni imara kiutendaji ukilinganisha na wachezaji wakongwe.
Kutathmini hali ya uzito wa mwili hakupo pekee kwa wachezaji wa soka, bali pia kwa jamii kiujumla. Itakumbukwa kuwa tatizo la unene ni moja ya vihatarishi vya kupata magonjwa yasiyoambukiza.
Hivi sasa kwenye jamii, muamko wa kufanya mazoezi mepesi unatokana na kulitambua tatizo la unene kuwa si zuri, kwani linahatarisha kupata magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kisukari na kiharusi.
Kufanya mazoezi na kuushughulisha mwili mara kwa mara katika maisha yetu ya kila siku ni moja ya njia rahisi za kuufanya mwili kuwa imara kiafya.
Mazoezi yanatufanya kuwa na afya bora, hivyo kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo ndiyo kinara wa kusababisha vifo vya mapema, huku gharama ya kutibu ikiwa kubwa.
Wengi wanaofanya mazoezi, watu wazima huwa na nia ya kukabiliana na unene au uzito uliokithiri, kwani hali hiyo husababisha matatizo ya kiafya katika kundi la utapiamlo. Ni kawaida watu walio wengi kufanya mazoezi, lakini hawajui wana uzito kiasi gani au kutofahamu unene alionao mtu upo katika kundi gani la uzito.
Ni muhimu sana kwa mtu yeyote yule, hata asiye mfanyaji mazoezi, kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uzito wa mwili ili pale unapozidi kiwango cha kawaida, hatua za mapema zichukuliwe.
Kitaalamu, zipo njia kadhaa ambazo mara nyingi hutumika kubaini unene uliokithiri au kujua mtawanyiko wa mafuta yaliyorundikana mwilini.
Njia hizo ni za kimahesabu kwa upimaji wa mzunguko wa kiuno tumboni na kugawa kwa urefu wa mwili, hujulikana kama waist circumference ratio. Njia ya pili ni waist-hip ratio, yaani uwiano wa mzunguko wa kiuno tumboni na mzunguko wa paja, na ya tatu ni Body Mass Index (BMI), ambayo ni uwiano au ulinganishaji wa uzito na urefu wa mwili.
Njia ya BMI ndiyo inatumika zaidi kutathmini uzito wa mwili kwa watu wazima. Siku ya leo nitaelekea zaidi njia hii, kwani ndiyo inatupa taswira ya unene mwilini.
Kwa kawaida hutumia fomula ya kihesabu kwa kugawa uzito katika kilo na urefu katika mita kipeuo cha pili. Mfano, mtu mwenye kilo 65 na urefu wa mita 1.5, BMI ni 70 gawa kwa 1.5 mara 1.5.
Kwa kutumia fomula, vipimo vya uzito na urefu, zao linalopatikana baada ya kukokotoa ndiyo hujulikana kama BMI. Njia hii inatuwezesha kubaini kama ni unene uliokithiri au ni uzito mdogo sana.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), BMI inatuwezesha kuainisha uzito wa mtu katika makundi matano. Jibu linalopatikana baada ya kukokotoa ndilo linatoa ainisho la uzito.
Kwa watu wazima, BMI ya 18.5–24.9 kitabibu ni uzito salama kiafya, 25.0–29.9 hapa ni uzito mkubwa, 30.0–39.9 hapa huhesabika kama ni unene na 40.0 kuendelea ni unene uliokithiri.
Endapo BMI itakuwa chini ya 18.5, maana yake ni kuwa mtu huyo ana uzito mdogo sana.
Katika BMI hapa tunaweza kutofautisha uzito uliokithiri, unene na unene uliokithiri, hivyo wataalamu wa afya huitumia njia hii kutathmini hatari za kiafya wanazoweza kuzipata watu baada ya matokeo ya BMI.
Njia hii ya BMI ni rahisi na haina gharama, ni njia ambayo inawezesha kubaini mrundikano wa mafuta mwilini na uzito uliokithiri kirahisi.
Kampuni za simu za smart zina mfumo laini ndani ya simu wenye kikokotozi cha BMI. Unachokifanya ni kujaza tu uzito (kg) wako na urefu wako, kisha inakupa majibu (m).
Ingawa BMI siyo njia ya moja kwa moja ya kupima mrundikano wa mafuta yote mwilini, lakini ni kiashiria muhimu kinachotuonyesha kuwa katika hatari ya kupatwa na magonjwa yasiyoambukiza.
CHUKUA HII
Kwa watu wa kawaida wasio wanamichezo, vizuri kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mepesi na kula vyakula visivyonenepesha kuanzia ngazi ya familia ili kuepukana na unene.
Wachezaji wa soka na wanamichezo wengine wanaishi maisha marefu yenye afya njema kutokana na wao kujihusisha moja kwa moja na mazoezi ya mara kwa mara, hivyo kutopata unene uliokithiri.