Karabaka ni maana halisi ya usajili wa mkopo
Muktasari:
- Hadi sasa ameshafunga mabao manne yanayomfanya awe kinara katika chati ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu na pia ameshatoa asisti za mabao mengine mawili.
SALEH Karabaka amekuwa wa moto sana pale JKT Tanzania ambako amekuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Hadi sasa ameshafunga mabao manne yanayomfanya awe kinara katika chati ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu na pia ameshatoa asisti za mabao mengine mawili.
Katika kikosi cha JKT Tanzania sasa hivi, Karabaka ametengeneza utatu fulani sumbufu unaowajumuisha pia Paul Peter na Edward Songo.
Huyu Paul Peter naye amefunga mabao matatu akifuata katika orodha ya wafumania nyavu akiwa sambamba na Peter Lwasa wa Pamba Jiji, huku Songo yeye amepachika bao moja tu.
Kijiweni mjadala mkubwa ni kwa huyu Karabaka maana yupo hapo JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba ambayo miaka miwili hapo nyuma alijiunga nayo akitokea huko Zanzibar.
Ndani ya JKT Tanzania, Karabaka anatimiza kwa ufasaha kile ambacho kinapaswa kufanywa na mchezaji wa mkopo. Anacheza kwa kujituma na anaonyesha shauku ya kutaka kuisaidia zaidi timu hiyo.
Na hiyo haikuanzia kwa maafande hao tu bali msimu uliopita alipokuwa pia akicheza kwa mkopo katika timu ya Namungo.
Anaonyesha anafahamu kwamba Simba inapomtoa kwa mkopo haimuonei bali inataka apate nafasi kubwa ya kucheza na kuimarisha kiwango chake, ili pale itakapomrudisha aweze kuhimili ushindani wa nafasi katika kikosi chao.
Karabaka anatoa somo kwa wachezaji wenzake kwamba wanapotolewa kwa mkopo, ni fursa kwao kujiboresha zaidi na sio adhabu.