Fahamu maajabu ya riadha kwa wanawake
Muktasari:
- Wengine hukimbia sio kwa sababu ya medali, bali 'kujinasua' kutoka kwenye vizingiti vya maisha. Hizo ni mbio dhidi ya mashaka, unyanyapaa, maumivu na hofu.
MIAKA ya karibuni taswira ya mwanamke anayeshiriki mbio au marathoni imekuwa zaidi ya picha ya mazoezi au ushindani na kugeuka kuwa matukio yanayoashiria nguvu nyingine waliyo nayo kinamama, uhuru na ujasiri.
Kila mara wanawake wanapojitokeza kushiriki katika mashindano mbalimbali ya riadha au mbio ndogo za kijamii kama wanatoa ujumbe mmoja kwamba kukimbia sio tu mchezo, bali ni njia ya kujiweka sawa kimwili, kiakili na kijamii. Kwa wanawake wengi, hasa wale wanaotoka katika jamii zenye mitazamo migumu kubadilika na kushiriki kwenye riadha ni tendo la kishujaa.
Wengine hukimbia sio kwa sababu ya medali, bali 'kujinasua' kutoka kwenye vizingiti vya maisha. Hizo ni mbio dhidi ya mashaka, unyanyapaa, maumivu na hofu.
Mwanariadha Zawadi Mushi ambaye amekuwa akishiriki mbio fulani mkoani Kilimanjaro kwa miaka mitatu mfululizo anasema:
“Nilianza kukimbia baada ya kupitia kipindi kigumu cha maisha. Nilipokuwa nikikimbia nilihisi kama naacha nyuma huzuni na maumivu. Kila hatua ya mbele ilikuwa ushindi juu ya jana yangu.”
Maneno yake yanawakilisha hisia za wanawake wengi wanaoona kukimbia kama tiba ya nafsi huku wengine wakikimbia wakiwa wametoka ofisini na wapo pia wanaofanya hivyo kutokana na changamoto za kifamilia au afya.
HARAKATI YA UWEZESHAJI
Kwa muda mrefu riadha ilionekana kama mchezo wa wanaume, lakini sasa wanawake wanazidi kuandika kurasa mpya katika historia wakianzia kung'ara kwenye mashindano makubwa hadi madogo, huku idadi yao ikiongezeka kwa kasi.
Mfano wa karibuni wa namna wanavyopiga hatua ni ule wa Magdalena Shauri, mwanadada aliyevunja mwiko wa ushindi kwenye Chicago Marathon, Marekani hivi karibuni alikoondoka na medali ya shaba akitumia muda wa 2:18:03 kushinda.
Lakini, takwimu zinaonyesha asilimia 40 ya washiriki wa Kilmanjaro Marathon wamekuwa ni wanawake likiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na miaka michache iliyopita. Hii ni ishara kwamba wanawake wanazidi kujiamini zaidi wakipiga hatua na kuamini katika uwezo wa kimwili na kiakili.
Kupitia mashindano hayo, wanawake wamekuwa wakipata fursa ya kuunganishwa na kuunganisha mitandao ya mawasiliano baina yao, jamii na hata makundi ya kisekta hasa ile ya uchumi ili kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Vilevile hupeana moyo na hata kuanzisha jumuiya ndogo za mazoezi. Miji kama Arusha, Dar es Salaam na Mwanza sasa imekuwa na vikundi vingi vya wanawake wanaokimbia kila asubuhi au jioni sio kwa ushindani, bali kwa ajili ya kujenga afya na kuimarisha udugu.
KAMA SAFARI YA MAISHA
Riadha ni mchezo unaofundisha nidhamu, uvumilivu na matumaini. Kila mwanamke anayekimbia ana hadithi yake kwani wapo wanaokimbia kusherehekea ushindi wa maisha kama vile kuyashinda maradhi au changamoto ya kifamilia. Lakini wapo wanaokimbia kuonyesha mfano kwa watoto wao wakiamini kwamba mama mwenye nguvu anaweza kuwalea watoto wenye ndoto.
Rehema Jonas aliwahi kushiriki mbio flani zilizofanyika karibuni na hapa anasema: “Nilianza kukimbia baada ya kujifungua. Nilihisi nimepoteza mwili wangu na furaha, lakini baada ya kuanza mazoezi ya kukimbia niligundua sio mwili pekee unaopona hata moyo na akili vinatulia.”
Kauli kama hiyo inaonyesha kwamba kukimbia ni zaidi ya mchezo. Ni safari ya kujipenda, kujikubali na kuponya nafsi na zaidi ni kwa mwanamke 'kuzungumza kimyakimya ndani ya nafsi' kupitia pumzi na mapigo ya moyo wake mwenyewe.
CHANGAMOTO NA USHINDI
Hata hivyo, safari ya wanawake katika dunia ya riadha haijawa rahisi kwani bado kuna changamoto za kijamii kama mitazamo hasi kwamba hawatakiwi kukimbia hadharani au kushiriki mashindano makubwa. Pia kuna changamoto za muda na majukumu ya kifamilia pamoja na kikazi ambazo mara nyingi zinawazuia wengi wao kufanya mazoezi.
Lakini, wanawake hao wameamua kubadilisha mchezo na kuufanya uwape kile wanachotamani kuwa nacho ambacho ni ushindi.
“Kila mwanamke anayevuta pumzi na kukimbia mita moja mbele ni mshindi,” anasema kocha Neema Katule, ambaye amekuwa akiwafundisha wanawake kukimbia jijini Dodoma na kuongeza: “Siyo lazima ushinde kwa muda, bali ushinde hofu ya kuanza.”
KIMWILI NA KIJAMII
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake wanaoshiriki katika riadha hupata nafuu kubwa ya msongo wa mawazo na huongeza kujiamini, kwani kukimbia huchochea kutoa homoni za furaha (endorphins) ambazo husaidia kupunguza huzuni na kuongeza nguvu ya kuamini katika nafsi.
Kijamii, mbio zimekuwa jukwaa la wanawake kuonekana na kusikika na ni njia ya kuonyesha kwamba nafasi ya mwanamke haipo jikoni pekee, bali pia kwenye barabara za mashindano.
Utafiti uliofanywa na Women's Sports Foundation (WSF), taasisi ya Uingereza inayoshughulika na tafiti na utetezi wa nafasi ya wanawake katika michezo unaonyesha kwamba kukimbia mara kwa mara kwa mwanamke kunaboresha afya ya akili.
Utafiti huo uliofanyika miaka saba iliyopita ulilenga kufuatilia ari na hamasa ya wanawake pamoja na faida wanazopata wanariadha wanawake pale wanaposhiriki riadha.
Lakini, King's College London, Uingereza na Chuo Kikuu cha Kentucky, Marekani walifanya utafiti wa kimataifa uliotaka kujua iwapo kuna uhusiano kati ya shughuli za kimwili na upunguzaji wa msongo wa mawazo pamoja na wasiwasi kwa wanawake kupitia riadha, ambapo walibaini kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wanaokimbia mara kwa mara wana kumbukumbu ya haraka katika mambo wafanyayo maishani mwao, hivyo wana kiwango kidogo cha hofu au wasiwasi katika mambo wanayofanya.
Pia walibaini kuwa ni chini ya asilimia 20 ya wanawake wanariadha wasiomudu kuwajibika kimwili katika mambo mbalimbali ya kijamii ikiwamo shughuli za kila siku na kwamba wengi wao wanapenda kujishughulisha na kazi mbalimbali kutokana na miili yao kuishi kwa mazoezi.