Balaa la miaka mitatu ya Injinia Hersi Yanga
JULAI 9, 2022, ilikuwa siku ya kihistoria kwa mashabiki na wanachama wa Yanga baada ya kumchagua Injinia Hersi Said kuwa rais wa klabu hiyo, huku akiwa ni mgombea pekee katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo, Wakili Ally Mchungahela alisema katika mkutano huo, “Kwa mujibu wa kanuni zetu za uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mgombea akiwa mmoja mkutano mkuu unapitisha azimio la mgombea huyo kuwa Rais.”
“Wajumbe mnaridhia Hersi Said kuwa Rais wa Klabu ya Yanga?” Alinukuliwa Mchungahela, huku wajumbe wakiitikia kwa kauli moja ya “ndioo”, kisha akarudia hadi mara tatu na kuonekana wanaunga mkono na ndipo Hersi akatangazwa Rais wa Klabu hiyo.
Kwa maana hiyo, kuanzia Julai 9, 2022 hadi leo, Hersi amefikisha miaka mitatu ya uongozi wake ndani ya Yanga na kupitia makala hii, Mwanaspoti inakuletea ahadi zake sita ambazo aliziahidi katika mkutano mkuu na kile alichokifanya hadi sasa.
MIUNDOMBINU YA KLABU
Ahadi kubwa aliyoanza nayo na kuwaahidi mashabiki na wapenzi wa Yanga, ilikuwa ya miundombinu, ambapo katika suala hilo aligusia ujenzi wa uwanja, marekebisho ya jengo la timu, kuendeleza vituo vya mazoezi vilivyopo Kigamboni Dar es Salaam.
Katika masuala hayo matatu, tayari mawili Hersi amefanikiwa kwa maana ya marekebisho ya jengo la timu, kuendeleza vituo vya mazoezi vilivyopo Kigamboni Dar es Salaam, ingawa suala la uwanja wenye uwezo wa kubeba mashabiki 20,000 ndio bado.
Hata hivyo, katika mazungumzo yake na mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kwenye makao makuu ya Yanga wakati wa paredi la ubingwa msimu wa 2024-2025, Hersi alinukuliwa akikiri moja ya ahadi ambayo anadaiwa ni suala zima la Uwanja wa Kaunda.
“Tulitakiwa kupata eneo kubwa ambalo lingefaa kujenga uwanja wa kisasa na miradi mingine mingi, tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kutupa ridhaa ya kuujenga kwa sababu mwanzoni mchakato huo ulikuwa bado unaendelea,” alinukuliwa Hersi.
MABADILIKO YA MUUNDO WA KLABU
Hersi anayeomba ridhaa ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwania Ubunge wa Jimbo la Kigamboni lililopo jijini Dar es Salaam, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ni miongoni mwa viongozi waliojiweka karibu na wanachama wa Yanga.
Klabu ya Yanga kupitia kwa wanachama walipitisha mfumo wa mabadiliko ya kiuendeshaji, ambapo Hersi alikiri kuyaendeleza kwa kuyasimamia kwa mujibu wa katiba, jambo linaloonekana kutimizwa kwa vitendo katika miaka yake hii mitatu ya uongozi.
KUIMARISHA UCHUMI WA KLABU
Katika ahadi hii, Hersi aligusia maeneo manne ya kuimarisha uchumi wa Yanga ambapo aligusia atafanikiwa suala hilo kwa kupitia miradi ya usajili wa wanachana, usajili wa mashabiki, kuvutia wadhamini mbalimbali na kuvutia pia wawekezaji.
Katika maeneo hayo, Hersi amefanikiwa zaidi usajili wa wanachama, usajili wa washabiki, kuvutia wadhamini mbalimbali na kuvutia pia wawekezaji, japo kuimarisha uchumi kwa kiasi kikubwa bado ni changamoto ingawa mwangaza unaonekana mbele.
Kuimarisha uchumi kwa klabu sio jambo jepesi na kwa mfano mzuri tu, katika mkutano mkuu wa Juni 9, 2024, klabu hiyo ilitangaza kupata hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa mujibu wa ripoti yake ya mapato na matumizi kwa msimu wa 2023-24.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Yanga uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ilionyesha ilipata Sh21.19 bilioni, lakini matumizi yalikuwa ni Sh22.29 bilioni.
Ukiangalia suala hilo, unaona ni wazi bado kuna safari ndefu kwa klabu zetu kujiendesha kisasa na kupata faida japo kwa uongozi wa Hersi kuzungumza hasara iliyopatikana kwa msimu wa 2023-24, ni kuonyesha ukakamavu na weledi kwa kiongozi.
KUJENGA KIKOSI IMARA
Katika hili, Hersi aligusia maeneo manne ambapo la kwanza ni kujenga kikosi imara kitakacholeta furaha kwa mashabiki wa Yanga kwa kuleta mataji mbalimbali kuanzia Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii na mashindano ya Kimataifa.
Katika maeneo hayo manne, Hersi amefanikiwa kwa maana kujenga kikosi imara cha kuleta pia ushindani, kwani tangu aingie madarakani amechukua Ngao ya Jamii mara mbili, mwaka 2022 na 2024, huku akichukua pia mara tatu mfululizo taji la Ligi Kuu Bara.
Katika Ligi Kuu Bara, Yanga imechukua ubingwa huo kuanzia msimu wa 2022-23, 2023-24 na 2024-25, wakati Kombe la TFF (FA) imelichukua pia mara tatu mfululizo, msimu wa 2022-23, 2023-4 na 2024-25.
Kwa ushindani wa ndani, Hersi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa japo changamoto imekuwa katika michuano ya kimataifa ya CAF, kwani kuna muda inafanya vizuri na kufika mbali, ingawa kuna msimu inaishia hatua ya makundi kama msimu wa 2024-25.
Licha ya kufanya vizuri michuano ya ndani, ila kwa msimu wa 2024-25, ilifanya vibaya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ambapo iliishia hatua ya makundi, ikiwa nafasi ya tatu kundi A kwa pointi nane, nyuma ya Al Hilal ya Sudan iliyoongoza.
Al Hilal iliongoza kundi na pointi 10, nyuma ya MC Alger ya Algeria iliyoshika ya pili na pointi tisa, huku TP Mazembe ya DR Congo ikiburuza mkiani kwa pointi zake tano, jambo linaloonyesha Yanga haikuwa na msimu mzuri kimataifa msimu huu.
Hata hivyo, chini ya Hersi, Yanga ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-24, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 25, tangu kikosi hicho kiliposhiriki mwaka 1998 na kutupwa nje mapema katika hatua ya makundi.
Pia, katika uongozi wa Hersi, Yanga ilifika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-23 na kukosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria kwa faida ya bao la ugenini, baada ya kufungwa nyumbani mabao 2-1, kisha kushinda ugenini 1-0.
TIMU ZA VIJANA NA WANAWAKE
Ahadi nyingine za Hersi alizoahidi ni kujenga kikosi imara cha kuleta ushindani kwa timu za vijana chini ya miaka 17, 20 na cha wanawake ya Yanga Princess, ingawa katika eneo hili bado imekuwa changamoto.
Kwa timu za vijana chini ya miaka 17 na 20, zimekuwa zikileta ushindani katika michuano mbalimbali kama ilivyo pia kwa Yanga Princess, ingawa kiu ya mashabiki wa kikosi hicho ni kuona hadhi ya timu ya wakubwa inaendana na zilizopo chini.
KUONGEZA USHIRIKIANO
Hersi alikuwa na maana ya kukuza ushirikiano baina ya klabu, wanachama, mashabiki zake, wadau mbalimbali ikiwemo idara za Serikali, sekta binafsi, waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla, jambo ambalo hadi sasa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Katika ahadi zote ambazo Hersi alizitoa mkutanoni, licha ya baadhi kuonekana tu kutokamilika, ni dhahiri kuna mwanga unaoonekana ndani ya kikosi hicho, huku akiwa ni mmoja wa viongozi wenye maono makubwa ya soka nchini hadi kimataifa.
Kuonyesha hilo, Desemba Mosi, 2023, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilizundua Chama cha Umoja wa Klabu za Afrika (ACA) huku ikimchagua, Hersi Said kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho chenye makao makuu Rabat, Morocco.
Uzinduzi huo ulifanyika Misri na kusimamiwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe.
Jessica Motaung wa Kaizer Chiefs aliteuliwa Makamu Mwenyekiti wa Hersi, huku Paul Basset wa Akwa United ya Nigeria akiteuliwa Makamu Mwenyekiti wa Pili.