Mazungumzo ya Salah na Besiktas yafikia mwisho
Muktasari:
- Mkurugenzi wa klabu hiyo, Onder Ozen, amesema walikuwa wamefikia hatua nzuri katika mazungumzo na Salah kabla ya masuala ya fedha kuibua mkwamo uliosababisha mazungumzo kusimama.
ANKARA, UBELGIJI: BESIKTAS imedai kusitisha rasmi mazungumzo ya kumsajili nyota wa Misri, Mohamed Salah, baada ya pande hizo kushindwa kufikia mwafaka wa kifedha licha ya kufanya mikutano mitatu.
Mkurugenzi wa klabu hiyo, Onder Ozen, amesema walikuwa wamefikia hatua nzuri katika mazungumzo na Salah kabla ya masuala ya fedha kuibua mkwamo uliosababisha mazungumzo kusimama.
Salah, ambaye sasa ni mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na Liverpool kwa makubaliano ya pande zote, alikuwa akihusishwa kwa karibu na kuhamia Besiktas. Rais wa klabu hiyo, Serdal Adali, awali alithibitisha kuwa walikuwa wakisubiri uamuzi wa mwisho kutoka kwa nyota huyo wa Misri.
Akizungumza na vyombo vya habari vya Uturuki, Ozen amesema Besiktas ilifanya kila juhudi kuhakikisha makubaliano yanapatikana, lakini ilisimama imara katika sera zake za kifedha.
"Tuliwasiliana na Salah na hata tukatengeneza mfumo wa kifedha kwa ajili ya dili hilo. Salah ni nyota wa dunia na mchezaji anayeheshimika. Tulikutana naye mara tatu kabla ya kuingia kwenye mazungumzo ya fedha," amesema Ozen.
Ameongeza kuwa kuanzia Julai 21, mazungumzo yalianza kwenda taratibu baada ya kuibuka kwa madai mapya kutoka upande wa mchezaji yaliyosababisha mkwamo katika mazungumzo.
"Besiktas ina sera zake na haiwezi kuzipuuza. Rais wetu aliweka msimamo wazi tangu mwanzo na hatukuwa tayari kuuvunja. Ofa yetu ya mwisho ipo mezani, lakini hatutatoa ofa nyingine."
Ozen pia alifichua kuwa wawakilishi wa Salah waliwaeleza kuwa wanaendelea kufanya mazungumzo na klabu nyingine, jambo ambalo linaonekana kuwa limechangia kusimama kwa mazungumzo hayo.
Kwa sasa, Salah mwenye umri wa miaka 34 anaendelea kuvutia maslahi kutoka kwa vilabu mbalimbali duniani. Miongoni mwa wanaomuwania ni klabu ya Sporting Kansas City ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), ambayo inadaiwa kumuwekea mezani ofa nono ya mkataba wa miaka miwili.
Hadi sasa, mustakabali wa mshambuliaji huyo bado haujafahamika, huku ikisubiriwa kuona atachagua kuendelea na soka la Ulaya au kuanza changamoto mpya nje ya bara hilo.