Sitaki tena urais -35
Muktasari:
- Zena akacheka. “Niliuona hapo hapo kwenye mlango nikafungua na kuingia.”
ILIKOISHIA
“Huu ufunguo uliofungulia mlango uliupata wapi?”
Zena akacheka. “Niliuona hapo hapo kwenye mlango nikafungua na kuingia.”
“Ufunguo niliondoka nao asubuhi.”
“Sasa kama uliondoka nao niliupataje?”
“Kwa kweli siwezi kujua uliupataje? Kwa maana nina maswali mengi, hata hiki chumba changu ulikijuaje?”
“Una maswali mengi kweli. Mimi nilifikiri ungefurahi kuniona chumbani mwako, kumbe unanikaribisha kwa maswali kama mhalifu niko polisi.”
“Hapana. Mbona nimefurahi sana kukuona, wewe hujui tu.”
SASA ENDELEA
“Nilijua ungekuja kunikumbatia na kunibusu na kuniambia umenimiss, badala yake ni maswali tu….”
Kwa jinsi nilivyoshituka kumuona humo chumbani mwangu, wazo la kwenda kumkumbatia na kumbusu halikuwemo kichwani mwangu kabisa. Yeye ndiye aliyenikumbusha.
“Samahani mpenzi,” nikamwambia na kwenda kukaa pembeni mwa kitanda. Alipoona nakaa akainuka na kukaa.
Nikajaribu kumpa tabasamu la bandia la muondoa wasiwasi.
“Nataka wewe ndiyo unifundishe mimi mapenzi,” nikamwambia.
“Mapenzi gani?”
“Yaani wewe ndio unifuate mimi unikumbatie na kunibusu….nijifunze.”
“Umri ulionao hujajua mapenzi bado?”
“Sijayajua.”
Zena akakunja uso. “Utaninyima raha. Nimekuja huku nipate raha, kumbe mwenzangu….”
Nikaupeleka mkono wangu wa kulia kukizunguka kiuno chake.
“Sio hivyo. Si unanifunza wewe,” nikamwambia. Akalegea. Akakilaza kichwa chake kwenye bega langu. Harufu ya nywele zake ikaja puani kwangu. Ilinisismua mwili mzima.
“Mbona wewe unanukia utamu namna hii?” Nikamuuliza.
“Kwa sababu najitunza. Nataka hata wewe unukie utamu.”
“Nitajifunza kwako.”
Ule msisimko ulionijia ulinifanya nimshike vyema na kumpiga kisi. Na yeye akanipa ushirikiano nikampiga kisi cha nguvu. Nilitaka nimuachie lakini alining’ang’ania.
“Raha sana,” akaniambia na kuniuliza,
“Lakini umeshakula?”
“Sijakula hadi sasa. Wewe umekula?”
“Sijakula pia.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Twende mahali ambapo tunaweza kupata chakula.”
“Kama wapi?”
“Hotelini.”
“Twende tutakodi bajaj.”
Zena akashuka kitandani na mimi nikashuka. Tukatoka. Ukumbini hakukuwa na mtu. Kila mkazi alikuwa chumbani mwake. Tukatoka nje na kwenda kukodi bajaj. Kitu ambacho kilikuwa kimenipa fahari ni kuona watu wakitutazama wakati tunapita.
Kusema kweli walikuwa wakimtazama Zena jinsi alivyopendeza na aliyekuwa akitembea kama msichana asiyejali kitu.
Tulikwenda kukodi bajaj tukaelekea katika hoteli moja iliyokuwa katikati ya jiji.
Tuliposhuka kwenye bajaj Zena aliniambia.
“Hapa watu wengi sana. Twende hoteli nyingine.”
“Hoteli gani?”
“Hoteli yenye utulivu. Hii haifai.”
Nikawaza kidogo kisha nikaikumbuka kivulini Hotel iliyokuwa pembeni kidogo mwa jiji.
“Tupeleke Kivulini Hotel,” nikamwambia mwendesha bajaj.
“Pesa itaongezeka.”
“Usijali.” Zena akadakia huku akitoa noti ya shilingi elfu kumi kutoka kwenye mkoba wake.
“Tukifika utanirudishia iliyobaki.”
Tukafikishwa katika hoteli hiyo. Ilikuwa hoteli tulivu na ya ghali. Kama pesa zako ni za madafu huwezzi kula chakula wala kunywa bia kwenye hoteli hiyo.
Kwa hiyo siku zote watu wanaoingia katika hoteli hiyo wanakuwa ni wachache na ni wale wanaojiweza.
Mwendesha bajaj akamrudishia Zena chenji yake tukaingia kwenye mgahawa wa hoteli. Kama kawaida tulikuta watu wachache waliokuwa wanakula na waliopendeza.
“Hapa panafaa sana.” Zena akaniambia tulipoingia ndani.
Tuliangaza meza tukaenda kukaa. Mhudumu alitufuata. Sote tukamuagiza chipsi na nusu kuku.
Tulipoletewa chakula hicho tukaanza kula.
“Mara ngapi umeshafika kwenye hoteli hii?” Zena akaniuliza.
“Nimefika mara nyingi lakini kula chakula hapa ni mara ya kwanza. Chakula chake ni ghali.”
“Wakati mwingine usiangalie ughali, angalia ubora wa kitu.”
“Chipsi kama hizi unaweza kuzipata kwa buku mbili sehemu zingine. Hapa unaweza kulipa elfu tano. Kwa watu wawili karibu elfu kumi.
“Si tatizo kama pesa unayo.”
“Pesa unaweza kuwa nayo lakini ukawa na mahitaji mengine muhimu.”
“Kwangu mimi hakuna mahitaji muhimu kama kula na kufurahisha roho yangu. Hata nguo ninazovaa si unaziona?”
“Ninaziona ni za ghali sana.”
“Lakini zenye ubora. Kila unapopita watu wanakutazama ingawa sipendi kutazamwa.”
Tuliendelea na mazungumzo hadi tulipomaliza kula. Zena akalipa pesa tukatoka.
“Sasa turudi nyumbani au siyo?” Zena akaniuliza.
“Turudi nyumbani.”
Tukaenda kupanda bajaj tena tukarudi nyumbani. Mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Nikagonga kwenye dirisha la rafiki yangu lililokuwa upande wa mbele.
“Nani?” Sauti ya rafiki yangu ikauliza kutoka chumbani mwake.
“Ni mimi Karim. Nifungulie mlango.”
“Subiri, ninakuja kukufungulia.”
Tulisubiri kwa sekunde chache tu mlango ukafunguliwa.
“Ingia,” nikamwambia Zena.
Zena akaingia na kuelekea kwenye mlango wa chumba changu. Nilitaka nimfahamishe yule rafiki yangu kuwa nimepata mgeni kutoka Dar lakini akawahi kuniuliza.
“Unazungumza na nani?”
“Ni huyo msichana ni mgeni wangu ametoka Dar. Nilikuwa nataka kukutambulisha.”
“Yuko wapi?”
“Una maana hujamuona huyo msichana aliyeingia?”
“Kuna msichana ameingia hapa?”
“Mmhh….” Nikaguna kisha nikaona nimuache. “Basi tutazungumza asubuhi.”
Nikaingia ndani na kufunga mlango. Rafiki yangu alikuwa anishi chumba cha kwanza upande ule uliokuwa na chumba changu ambacho kilikuwa cha katikati. Rafiki yangu huyo aliingia chumbani mwake na mimi nikaenda kwenye mlango wa chumba changu ambapo Zena alikuwa amesimama akinisubiri.
Nikatoa funguo na kufungua mlango tukaingia ndani.
“Ulikuwa unasemeshana nini na yule mwenzako?” Zena akaniuliza tukiwa chumbani.
“Alikuwa ananiuliza nazungumza na nani, nikamwambia nilikuwa nazungumza na huyu msichana aliyeingia. Nilikuwa nataka kukutambulisha kwake kwa vile ni rafiki yangu lakini akaniambia eti hajakuona.”
“Unataka unitambulishe kwa rafiki yako kwani umeshanioa?”
“Sijakuoa lakini kwa vile yule ni rafiki yangu niliona si vibaya kukutambulisha.”
“Sasa mbona hukumtambulisha?”
“”Amsema eti hajakuona wakati unaingia yuko kando ya mlango.”
“Alivyokwambia ni sawa. Hajaniona. Na ni kwa sababu hujanioa.”
Kwa vile nilishazoea kuona vituko vyake tangu tukiwa Dar, nikaona ninyamaze.
Wakati huo Zena alikuwa akivua nguo zake na kuzitundika.
“Hebu washa feni. Wewe huoni joto?”
Nikaenda kuwasha feni. Zena alivua nguo zote akabakisha nguo ya ndani na sidiria. Na mimi nikaona nivue zangu. Nikabakisha bukta niliyokuwa nimevaa ndani.
Zena alikuwa amekaa kitandani akipepewa na feni.
“Njoo hapa,” akaniita pale kwenye kitanda.
Nikaenda kukaa naye. Sasa ngozi yake ya mwili niliiona kwa karibu. Alikuwa ameota vinywelea tumboni na kifuani kwake kama mwanaume. Huko mgongoni pia aliota vinywelea kwenye msitari wa uti wa mgongo.
“Kwa vile hujanioa huwezi kunifaidi mimi.” Zena akaniambia.
Kama ilivyotokea nilipolala naye Dar ikanitokea tena chumbani mwangu. Sikujua kama usingizi ulinipitia ghafla au nilipotewa na fahamu kwani baada ya kuniambia hivyo sikujielewa tena.
Nikaota nikifanya mapenzi na Zena tukiwa ufukweni mwa bahari. Baada ya hapo tukaenda kuoga maji ya bahari.
Nilizinduka usiku wa manane nikiwa nimelala kitandani peke yangu. Zena sikumuona. Taa ilikuwa inawaka na nguo za Zena zilikuwepo mahali pale pale alipozitundika.
Wakati ninajiuliza Zena yuko wapi nikasikia sauti yake nyuma ya nyumba. Sauti ilikuwa ikipitia kwenye dirisha ikisema.
“Nimeshakwambia nenda katekeleze kazi niliyokutuma. Usirudi tena kunisumbua. Mume wangu mtarajiwa amelala, sitaki kumwamsha.”
Sikujua Zena alikuwa akizungumza na nani lakini kile kitendo cha kumsikia akizungumza nyuma ya nyumba usiku ule kilinishitua sana. Nikanyamaza kimya na kusikiliza. Sikusikia tena sauti yake. Nikaona ile taa ya chumbani inazima yenyewe na hapo hapo nikapitiwa na usingizi tena.
Nilipolala nikaota tena ninafanya mapenzi na Zena ufukweni mwa bahari.
Zena ndiye aliyeniamsha asubuhi. Nilikuwa nimelala naye kitandani.
“Si unakwenda kazini?” Akaniuliza.
“Ndiyo ninakwenda kazini.”
“Amka basi uende ukaoge.”
“Wewe je?”
“Mimi utaniacha humu humu chumbani.”
“Kuoga je?”
“NItaoga usiku.”
Nikashuka kitandani na kujifunga taulo. Nilitoka uani nikapiga mswaki na kuoga kisha nikarudi chumbani mwangu. Zena alikuwa bado amejinyoosha kitandani.
Nilivaa nguo zangu. Nilipokuwa tayari nikamuuliza Zena.
“Kwahiyo?”
“Wewe nenda kazini kwako, tutaonana utakaporudi.”
“Sasa utakula nini?”
“Usijali Karim, nitakula tu.”
“Kwa kawaida nikitoka asubuhi ninarudi jioni lakini kwa sababu yako nitakuja mchana kukuangalia.”
“Sawa. Njoo tu.”