Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyoshi: Napiga pamba za milioni tatu kabla ya shoo

Muktasari:

  • Kwa mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi na rais wa Bogoss Musica, Nyoshi El Saadat, maandalizi hayo yana gharama kiasi cha kutumia hadi Sh3 milioni kwa ajili ya mavazi na viatu katika shoo moja. Akizungumza na Mwanaspoti baada ya shoo ya Werrason, Nyoshi anafunguka mambo anayoyafanya kabla ya kupanda jukwaani. Twende naye!

Kupanda jukwaani na kutoa burudani inayowafurahisha mashabiki kunahitaji maandalizi ya kutosha kuanzia mwonekano wa msanii, utunzaji wa sauti hadi utayari wa wanamuziki wanaomsindikiza.

Kwa mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi na rais wa Bogoss Musica, Nyoshi El Saadat, maandalizi hayo yana gharama kiasi cha kutumia hadi Sh3 milioni kwa ajili ya mavazi na viatu katika shoo moja. Akizungumza na Mwanaspoti baada ya shoo ya Werrason, Nyoshi anafunguka mambo anayoyafanya kabla ya kupanda jukwaani. Twende naye!


Mwanaspoti:  Kabla ya kupanda jukwaani, huwa unaanza na maandalizi gani?

Nyoshi: Kwanza kabisa huwa naanza na maandalizi ya mwonekano wangu. Naenda saluni kutengeneza uso na ndevu ili kuhakikisha ninakuwa nadhifu kabla ya kwenda jukwaani. Kwa msanii, mwonekano ni sehemu ya kazi, hivyo siwezi kuupuuza.

Mwanaspoti: Kwa shoo moja, maandalizi ya mavazi yanakugharimu kiasi gani?

Nyoshi: Kwa siku moja ya shoo natumia hadi Sh milioni 3, kuanzia viatu hadi mavazi. Nina viatu vya aina mbalimbali, vingine vina thamani ya hadi Sh800,000. Napenda kuvaa vizuri kwa sababu jukwaa linahitaji heshima na mwonekano unaoendana na burudani ninayoitoa.


Mwanaspoti: Unailindaje sauti yako kabla ya shoo?

Nyoshi: Sauti ndiyo mtaji wangu, kwa hiyo lazima niitunze. Saa chache kabla ya shoo huwa najiepusha na vitu vya baridi na vyenye mafuta mengi. Natumia maji ya uvuguvugu na asali kidogo. Pia nafanya mazoezi ya sauti kwa kuipandisha na kuishusha ili iwe tayari kwa kazi ya jukwaani.


Mwanaspoti: Kabla ya kuanza kutumbuiza, huwa unajiandaa vipi kiakili?

Nyoshi: Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi nyingine ya kufanya kazi. Baada ya hapo natenga takribani dakika 15 za kukaa kimya ili kupata utulivu wa akili. Katika muda huo napitia pia orodha ya nyimbo nitakazozitoa ili nijue namna ya kupanga burudani ya usiku huo.


Mwanaspoti: Kama kiongozi wa Bogoss Musica, unahakikishaje bendi iko tayari?

Nyoshi: Tunafanya mazoezi ya pamoja kabla ya shoo ili kila mwanamuziki ajue nafasi yake. Kuanzia wapiga gitaa, tumba na vyombo vingine hadi waimbaji, kila mmoja anapaswa kujua wajibu wake. Pia tunazingatia nidhamu na muda. Wanamuziki wanatakiwa kufika mapema, kisha tunafanya ukaguzi wa sauti ili kuhakikisha kila kitu kiko sawa kabla ya kuanza.

Mwanaspoti: Unapokuwa jukwaani, unatumia mbinu gani kuhakikisha mashabiki hawachoki?

Nyoshi: Kwanza huwaangalia mashabiki na mazingira ya eneo husika ili nijue namna ya kuanza nao. Sipendi kuimba huku nikitazama upande mmoja tu. Nawasiliana nao kwa macho, maneno na kuwashirikisha katika baadhi ya nyimbo. Pia nasimamia mpangilio wa nyimbo, mabadiliko ya mapigo na wakati wa sebene kupanda kasi.


Mwanaspoti: Unawezaje kuhakikisha wanamuziki wanafuata mabadiliko ya muziki ukiwa jukwaani?

Nyoshi: Tunatumia ishara za mikono na miondoko ambayo wanamuziki wanaielewa. Hii inawasaidia kujua wakati wa kubadilisha mapigo au kuongeza kasi ya sebene. Kiongozi wa bendi anatakiwa kuwa makini kwa sababu ndiye anayesimamia mwelekeo wa burudani.


Mwanaspoti: Kuna umuhimu gani wa kuimba sauti ya moja kwa moja katika muziki wa dansi?

Nyoshi: Ni muhimu sana kutoa sauti ya moja kwa moja badala ya kutegemea sauti zilizorekodiwa. Muziki wa dansi una uhai wake, hasa kwenye sebene na mitindo ya kucheza. Mashabiki wanataka kuona na kusikia uwezo wa mwanamuziki jukwaani.

Mwanaspoti: Kwa ujumla, ungependa mashabiki waelewe nini kuhusu maandalizi ya shoo?

Nyoshi: Ningependa waelewe kuwa muziki wa dansi si kelele. Ni sanaa inayohitaji maandalizi, heshima na kazi kubwa. Kila ninachokifanya kabla ya kupanda jukwaani kina lengo moja, kuhakikisha mashabiki wanapata burudani inayostahili.