Frida, Master J wafunguka albamu mpya za wasanii
Muktasari:
- Upepo huo unaonekana kubadilika huku baadhi ya wasanii wakubwa wameanza kurejea kwenye utamaduni wa kutoa albamu, akiwemo Harmonize, Aslay na kundi la Navy Kenzo wakiwa miongoni mwa majina yaliyoweka nguvu kwenye eneo hilo.
KWA miaka ya hivi karibuni, muziki wa Bongofleva ulionekana kutawaliwa na mfumo wa kutoa singo moja baada ya nyingine. Msanii anatengeneza wimbo, anautangaza, unafanya vizuri kwa muda, kisha anatoa nyimbo.
Upepo huo unaonekana kubadilika huku baadhi ya wasanii wakubwa wameanza kurejea kwenye utamaduni wa kutoa albamu, akiwemo Harmonize, Aslay na kundi la Navy Kenzo wakiwa miongoni mwa majina yaliyoweka nguvu kwenye eneo hilo.
Swali linalobaki ni moja, kwa nini albamu zimeanza kupata nafasi tena wakati singo zinaonekana kuwa rahisi kusambaa hasa kwenye mitandao ya kijamii?
ALBAMU NI ‘CV’
Rapa maarufu nchini Frida Amani anaamini albamu si suala la kufuata mkumbo, bali ni sehemu muhimu ya safari ya msanii anayetaka kujenga jina lake kwa muda mrefu.
Kwa mtazamo wake, msanii mwenye albamu ana nafasi kubwa ya kuonyesha uwezo wake kwa upana zaidi kuliko yule anayejulikana kupitia wimbo mmoja. “Kutoa album sio trend, ni lazima kwa msanii na ni kitu ambacho kinakufanya unakuwa official,” alisema Frida.
Anaongeza kuwa albamu inaweza kuwa kama wasifu wa kazi wa msanii, hasa anapotaka kuingia kwenye soko kubwa zaidi.
“Kwenye muziki album ndio representation yako… ukipeleka pale ndiyo CV yako kwamba inaelezea huyu amefanya hivi na hivi,” alisema Frida.
Kwa maana hiyo, albamu haibebi nyimbo pekee, bali pia inaonyesha uwezo, ubunifu na mwelekeo wa msanii.
STREAMING NA CHACHU YA PESA
Kwa upande mwingine, mtayarishaji wa muziki mkongwe Master J anaona suala hilo pia lina upande wa kibiashara.
Katika zama ambazo muziki unasikilizwa zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali, msanii mwenye nyimbo nyingi ana nafasi ya kupata wasikilizaji wengi zaidi kuliko anayesukuma kazi moja pekee.
“Hela ya streaming ni ndogo sana, kwa hiyo ni muhimu uwe na nyimbo nyingi ili watu waweze kusikiliza nyimbo zako nyingi, ambacho kinaongeza mapato yako,” alisema Master J.
Kwa mfano, shabiki anayesikiliza albamu yenye nyimbo 10 anaweza kuendelea kusikiliza kazi za msanii huyo kwa muda mrefu badala ya kuishia kwenye wimbo mmoja.
JUKWAANI NDIPO TOFAUTI ILIPO
Master J pia anaona albamu ikimsaidia msanii kwenye upande wa maonyesho ya moja kwa moja.
Anasema promota anapomtafuta msanii kwa ajili ya tamasha, uwezo wa kuwa na nyimbo nyingi za kuimba jukwaani unaweza kuongeza thamani yake.
“Kama unakuja tu kuimba mmoja wa dakika mbili, nitakulipa hela ndogo. Lakini kama unakuja kuimba nyimbo 10 unaweza ukaendesha show ya nusu saa,” alisema Master J.
Hivyo, msanii mwenye katalogi kubwa anaweza kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya shoo ndefu na kuwapa mashabiki burudani ya kutosha.
SI WAKONGWE TU
Mkakati huo hauishii kwa mastaa wenye majina makubwa, Master J anawashauri pia wasanii wakongwe kuendelea kutoa kazi mpya ili waendelee kuwasiliana na kizazi cha sasa.
Kwa wasanii wanaochipukia, ushauri wake ni kuanza na singo ili kujenga jina, kisha kuongeza kasi kwa EP au albamu.
Hatimaye, kinachoonekana ni kwamba Bongofleva haijaachana kabisa na singo, bali wasanii wameanza kuona umuhimu wa kuwa na hazina kubwa ya muziki.
Albamu sasa inakuwa zaidi ya mkusanyiko wa nyimbo, ni wasifu, mtaji wa streaming na silaha ya msanii jukwaani.
Kwa msanii anayetaka kujenga jina na si kutamba kwa wimbo mmoja pekee, safari kutoka singo hadi albamu inaweza kuwa hatua muhimu ya kuthibitisha uwezo wake.