Ukame wa mabao wamtesa Niyonzima
Muktasari:
Niyonzima amejiunga na Simba msimu huu akitokea kwa mahasimu wao, Yanga hajafanikiwa kufunga bao tangu kuanza kwa msimu, lakini amekuwa ni mchezaji anayependwa na kukubalika kwa mashabiki wa Simba.
Dar es Salaam. Kiungo Haruna Niyonzima amewaomba mashabiki Simba waendelee kumuombea dua ili aweze kurudi katika ubora wake wa kuzifumania nyavu.
Niyonzima amejiunga na Simba msimu huu akitokea kwa mahasimu wao, Yanga hajafanikiwa kufunga bao tangu kuanza kwa msimu, lakini amekuwa ni mchezaji anayependwa na kukubalika kwa mashabiki wa Simba.
"Nilikuwa katika kipindi kigumu kidogo cha kuzoeana na wachezaji wenzangu, lakini nafarijika sasa nimeanza kuzoea mazingira ndani ya Simba.
"Siku zote uwa naamini mimi ni mchezaji mzuri, lakini siwezi kuwa mzuri bila ushirikiano na wenzangu, hakuna mchezaji wa aina hiyo.
"Nimekuja Simba kufanya kazi, najua mashabiki wanatamani sana kuona 'makeke' yangu uwanjani, lakini wasiwe na wasiwasi siku si nyingi mambo yatakuwa mazuri," alisema mchezaji huyo ambaye aliondoka Yanga ikiwa bado inamhitaji.
Kiungo huyo aliyepewa jina la fundi alisema tayari amekwishaanza kuzoea upepo ndani ya Simba na kusisitiza kwamba siku si nyingi ataanza kufanya vizuri.
Akizungumzia mchezo wao wa kesho Jumapili dhidi ya Stand United, Niyonzima alisema hiyo ni mechi ambayo hawatakiwi kupoteza.
"Tuko vizuri, hiyo ni mechi ambayo hatutakiwi kupoteza, tunaomba Mwenyezi Mungu atuamshe salama siku hiyo tupambane kwa ushindi kwani tumejifua kwa ajili ya kupata matokeo," alisema kiungo huyo.