Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Salamba, Kaheza tishio jipya Simba

Dar es Salaam. Safu mpya ya ushambuliaji ya Simba, imetoa taswira ya upana wa kikosi kitakavyokuwa kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba ambao wamelenga kuongeza upana wa wigo wao wa safu  ya ushambuliaji iliwasajili Adam Salamba (Lipuli) , Marcel Kaheza (Majimaji) na Mohammed Rashid (Tanzania Prisons) ili kukidhi mahitaji hayo.

Washambuliaji hao, walianza kukitumikia kikosi hicho kwenye michuano ya Sportpesa nchini Kenya, lakini walionekana kushindwa kuonyesha ubora wao.

Kaheza na Salamba wameonekana kuanza kuelewana kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la Kagame kwa kuifunga mabao muhimu timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa Simba dhidi ya Dakadaha.

Katika mchezo huo uliochezwa jana Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 mbele ya Wasomalia hao.

Kaheza ambaye alitumika kwenye mchezo huo kama winga wa aliyekuwa anatokea pembeni ndiye aliyekuwa wa kwanza kuifungia Simba bao la kwanza kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika ya tisa ya mchezo.

Bao la pili kwa Simba lilifungwa na Adam Salamba kwa shuti baada ya kuchongwa krosi na beki wa kulia, Shomary Ally.

Kabla ya mapumziko Simba ilijipatia bao la tatu kupitia kwa Rashid Juma ambaye alikuwa akicheza winga ya upande wa kushoto.

Salamba na Kaheza ambao walianza kwenye eneo la ushambuliaji kwenye kipindi hicho cha kwanza japo mmoja alikuwa akitokea pembeni walionekana kuwa na maelewano mazuri.

Mara kadhaa Salamba alitumia ukubwa wa mwili wake kushuka chini na kusaidia kukaba pindi walipokuwa wanapoteza mipira huku nafasi yake juu ikizibwa vizuri na Moses Kitandu aliyekuwa akicheza namba 10.

Upande wake Kaheza naye alikuwa akisogea kwenye eneo la kiungo na kumuongezea nguvu, Mzamiru Yassin.

Wakati Salamba na Kaheza wakicheza vizuri kipindi hicho cha kwanza, Pascal Wawa ambaye naye ni usajili mpya kwenye kipindi hiki cha usajili alionyesha kiwango cha juu kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Kipindi cha pili, Simba iliendelea kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa huku wakionekana kuwa na uhai zaidi kwenye eneo la kiungo ambalo alikuwa akicheza Mzamiru na mkongwe Mwinyi Kazimoto.

Salamba aliipatia bao la nne Simba kwa kuachia shutu kali nje ya kumi na nane lililomshinda mlinda lango wa Dakadaha, Mustaf Hussein.

Simba ilifanya mabadiliko kadhaa kwenye kipindi hicho cha pili kwa kuwatoa, Kaheza, Kitandu, Rashid huku nafasi zao zikichukuliwa na Mohammed Rashid, Said Ndemla na Abdul Hamis.

Mabadiliko hayo yaliiendelea kuifanya Simba kumiliki mpira kwa asilimia kubwa huku ikilisakama lango la Dakadaha hadi mwisho wa mchezo.

"Tulicheza vizuri japo kuna makosa madogo ambayo yalikuwa ya kifanyika, nimefurahishwa na namna ambavyo washambuliaji wangu wamecheza, bado tuna muda wa kuendelea kuwa pamoja kwa hiyo kunauwezekano wa kuendelea kuona vitu vizuri kutoka kwao," alisema Masoud Djuma.