Mauzo tiketi Yanga, Simba yaanza kwa kusuasua
Muktasari:
- Mashabiki wengi wa Tanzania wamekuwa na utaratibu wa kununua tiketi katika siku ya mwisho
Dar es Salaam. Mashabiki wa Simba na Yanga wameendelea kuishi kwa mazoea wakisubiri kununua tiketi siku za mechi, jambo ambalo limesababisha mauzo ya tiketi za mchezo wa watani hao wa jadi kesho Jumamosi kukwama.
Simba na Yanga zinakutana kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wenye uwezo wa kubeba mashabiki 22,000 tu, lakini mpaka majira ya saa 4.18 asubuhi ya leo Ijumaa ni tiketi 2,012 tu zilizouzika. Tiketi hizo zilianza kuuzwa Jumatatu ya wiki hii.
Mchezo huo wa watani wa jadi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 unachezwa kwenye uwanja wa Uhuru ambao unawanyima fursa mashabiki 38,000 kuutazama ukilinganisha na ule wa Uwanja wa Taifa ambao ni mkubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema wanasubiri mpaka leo Ijumaa jioni kuona hali ya mauzo inakwendaje ili kuona kama kesho Jumamosi kutakuwa na usumbufu mkubwa kwenye ununuzi.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Clement Sanga ameteua Kamati mpya ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.
Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ambayo ataiongoza yeye mwenyewe ni Shani Mligo (Makamu Mwenyekiti), Boniface Wambura (Katibu), Issa Batenga, Leslie Liunda na Wakili Saleh Njaa.
Wengine ni Dr Ellyson Maeja, George Malawa, Isaac Chanji, Baruan Muhuza, Mbakileki Mutahaba na Ally Mayay.
Kamati hiyo ya TPLB ndiyo inayoshughulikia uendeshaji na usimamizi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na Ligi Daraja la Pili (SDL).
Pia, Mwenyekiti ameteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya TPLB. Wajumbe hao ni Kanali Charles Mbuge ambaye ni Mwenyekiti wa timu ya Ruvu Shooting, na Abuu Changawa (Majeki).
Kwa mujibu wa Ibara ya 28(vi) ya Kanuni za Uendeshaji (Governing Regulations) za TPLB, Mwenyekiti ana nafasi ya kuteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Uongozi.