Mashuti yamuweka benchi Tshishimbi

Muktasari:

Tshishimbi alipata maumivu hayo juzi jioni katika mazoezi ya kupiga mashuti makali zoezi ambalo kila mchezaji alitakiwa kufanya ukiondoa makipa.

Morogoro. Kiungo wa kigeni wa Yanga, Pappy Tshishimbi amelazimika kuwa nje katika ratiba ya kikosi hicho jana baada ya kupata maumivu.

Tshishimbi alipata maumivu hayo juzi jioni katika mazoezi ya kupiga mashuti makali zoezi ambalo kila mchezaji alitakiwa kufanya ukiondoa makipa.

Kiungo huyo baada ya kumaliza zoezi hilo alishindwa kuendelea na ratiba nyingine na alijiengua kwenye kikosi kwenda kutibiwa jereha hilo na daktari wa timu huyo Edward Bavu.

Akizungumza na gazeti hili Kaimu Ofisa Habari wa Yanga, Godlisten Anderson alisema maumivu hayo sio makubwa kwa mujibu wa daktari wao na tayari nyota huyo amepata matibabu na afya yake inaendelea vyema.

Anderson alisema mbali na Tshishimbi, beki Kelvin Yondani anaumwa malaria na wachezaji wote wawili walikosa mechi ya kwanza ya kujipima nguvu dhidi ya Tanzanite Academy.

“Nikweli Tshishimbi amepata maumivu ya nyama, lakini jana (juzi) alitibiwa na yuko sawa, lakini madakari wamemtaka apumzike leo (jana) ili awe vizuri zaidi hata Yondani naye ameamka na malaria lakini anaendelea vyema,”alisema Anderson. Yanga imeweka kambi mkoani hapa kujiandaa na mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.