Martin:Zahera mbona safi tu
Muktasari:
- Martin alisema licha ya kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ameongeza vitu katika uchezaji kupitia mazoezi ya Zahera.
Dar es Salaam. Winga wa Yanga, Emmanuel Martin amezidi kuvutiwa na programu zinazoendeshwa na kocha wake mkuu Mwinyi Zahera kadri siku zinavyokwenda.
Martin alisema licha ya kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ameongeza vitu katika uchezaji kupitia mazoezi ya Zahera.
"Amekuwa akihitaji tushambulie kwa nguvu na kujilinda, kuwa wepesi kupeleka mashambulizi hilo ndio kubwa katika upande wangu, mazoezi yameniongezea wepesi," alisema Martin.
Akizungumzia changamoto ya namba, alisema jambo hilo linatokea katika timu inayokuwa na wachezaji wengi wenye ushindani.
"Uwepo wa Mrisho Ngassa sio kwamba unanifanya nisicheze lakini kilichopo ni kwamba timu ina kikosi kipana kwahiyo yoyote anayecheza ana uwezo wa kuisaidia timu, hilo ni jambo zuri," alisema.