Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manji ashtua mastaa Yanga

Yusuf Manji

RUDINI Yanga kumenoga jamani! Yanga jana jioni imetua jijini Dar es Salaam, ikitokea kambini kule Morogoro huku wachezaji wake wakiwa na mzuka kwelikweli kutokana na taarifa njema walizopewa.

Leo saa 1:00 usiku jeshi zima la Mwinyi Zahera litakuwa Uwanja wa Taifa kuwakabili USM Alger ya Algeria kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika. Huo utakuwa mchezo wa mwisho wa nyumbani kwa Yanga na itabakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.

Hata hivyo, macho ya mashabiki wa Yanga na hata wale watani zao, Simba yatakuwa jukwaani kuwaona watu wawili maarufu kwelikweli, lakini kuna mmoja ndio atashtua zaidi na tayari ameshapandisha mzuka wachezaji.

Yanga haina nafasi kabisa ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na wanasaka heshima pamoja na kusaka nafasi ya tatu, ambayo itawafanya kuvuna mkwanja wa maana.

Kama Yanga itashinda mchezo wa leo kisha kwenda kufanya kweli nyumbani kwa Rayon Sport pale Kigali, Rwanda, itafikisha pointi saba ambazo zitaifanya kushika nafasi ya tatu huku ikiomba zaidi USM Alger na Gor Mahia ambao wako juu, watoe sare ama kupoteza mbili.

Akili hiyo ikawafanya mabosi wa Yanga kutimiza matakwa ya makocha wao na kuipeleka timu kambini na taarifa, kikosi kimeiva na kipo tayari kwa mapambano.

Ikiwa Moro mpaka jana asubuhi Yanga imefanya mazoezi makali chini ya Zahera, ambaye ametamba vijana wake wako tayari kwa shughuli.

Sasa ishu iko hivi. Yanga imetangaza mgeni rasmi kwenye mchezo wa leo ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo ambaye ndiye atawaongoza mashabiki wa Jangwani kwenye mchezo huo na ni mdau mkubwa wa michezo.

Hata hivyo, mzuka zaidi ni kuwa Mwenyekiti wa timu hiyo Yusuf Manji, amethibitisha kuwa atakuwa uwanjani kushuhudia jeshi lake.

Taarifa hizo za Jenerali Mabeyo ukiongeza na uwepo wa Manji, zikatua kambini huko Morogoro na wachezaji wakala yamini wakipeana mzuka kuwa ‘Jamani twendeni tukafie kwa Mchina-Uwanja wa Taifa’.

Nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul akiwa na kiongozi wake Kelvin Yondani ndiyo waliofanya kazi hiyo wakiwaambia wenzao, huu ndio muda wa kufanya kweli.

Abdul ameliambia Mwanaspoti taarifa za uwepo wa Jenerali Mabeyo na Manji uwanjani hapo, zimewashtua na jana asubuhi walifanya mazoezi makali kila mchezaji akipambana kuwania namba katika kikosi cha kwanza.

Ushindani huo ukamshtua Kocha Zahera, ambaye hakuelewa kinachoendelea hadi alipotonywa wakubwa wanakwenda uwanjani kushuhudia vijana.

Zahera ameliambia Mwanaspoti baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya USM Alger ugenini kwa mabao 4-0, huu ni wakati wa kulipa kisasi.

Amesema wapinzani wao hao walikutana na Yanga iliyoundwa na ‘watoto’ kwa wachezaji wengi wazoefu kukosekana na leo mziki kamili utashushwa uwanjani.

Alisema kurejea kwa Pappy Kabamba Tshishimbi, Yondani, Kakolanya huku Deus Kaseke na Heritier Makambo wakiongezeka anaamini watapata matokeo mazuri.

Mkongomani huyo alisema USM Alger ni timu nzuri na anafahamu ubora wao uwanjani, lakini hilo haliwezi kuwazuia vijana wake kupata ushindi.

“Tumekuwa na muda mzuri wa maandalizi, mechi ya kwanza tulipoteza dhidi ya hii timu lakini tulipokuwa kule tulikuwa na wachezaji wengi wachanga wasio na uzoefu,” alisema Zahera.

“Tumeunda timu kamili wapo wazoefu kama Yondani, Papy na wengine kesho (leo) watakuwepo ukiongeza na hawa wapya nafikiri mambo yatakuwa tofauti kabisa.”

Manji ateta na wachezaji, viongozi Yanga

Wakati mambo yakizidi kuwa moto, Manji amekutana na wachezaji wa Yanga na Kamati ya Mashindano ya Yanga kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo mpambano wa leo kukamilisha ratiba dhidi ya USM Alger.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika alisema kamati yake ilifanya kikao na mwenyekiti wao, ambaye alikuwa nje ya soka kwa muda mrefu na amewahakikishia atakuwepo uwanjani hapo leo.

Mwanaspoti pia linafahamu jana usiku, Manji alipata chakula cha usiku pamoja na wachezaji na viongozi, pia alizungumza na wachezaji.

“Manji ameahidi atakuwepo uwanjani leo hivyo, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuiona timu na kumwona kiongozi wao na tuna imani kubwa kufika kwake ni mwanzo mzuri kwetu na baada ya hapo tutafanya mengine zaidi ya kimaendeleo,” alisema Nyika.

Naye Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema kikosi na wachezaji wote ambao wana leseni ya kushiriki mashindano hayo wapo fiti na jukumu litabaki kwa Zahera kuamua nani wa kumtumia katika mechi hii.

Ten alisema viingilio vitakuwa Sh3,000, kwa mzunguko VIP B na C itakuwa Sh7,000 wakati VIP A itakuwa Sh10,000 na tuna imani viingilio rahisi kwa kila mpenzi wa soka kuja kushuhudia burudani.

“Mgeni rasmi kama kawaida atakuwa Jenerali Venance Mabeyo, pia tulimwalika Rais wetu John Pombe, ambaye amekuwa akitupa ushirikiano wa kutosha, lakini hataweza kuhudhulia kutokana kuwa na majukumu mengine ya kitaifa,” alisema Ten.

Yanga imepata mzuka huo ikiwa pia inajiandaa na michuano ya Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Agosti 22 na itaanza kukipiga na mabingwa wa kombe la FA, Mtibwa Sugar ya Morogoro.