Lwandamina apata msiba agoma kuondoka
Muktasari:
- Yanga na Simba zitaumana Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru
Shinyanga. Kocha George Lwandamina amepata taarifa za msiba ya mtoto wa dada yake,lakini hatoondoka mpaka baada ya mechi dhidi ya Simba na Singida United.
Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti.co.tz, Lwandamina alisema alipokea simu ya msiba wa mtoto huyo muda mfupi kabla ya timu yake kuingia uwanjani kuumana na Stand United.
Lwandamina alisema licha ya kupokea taarifa hizo hataweza kuiacha timu yake ikiwa katika vita kubwa ya kukutana na Simba na sasa ataingia kambini kuhakikisha anamaliza mechi hiyo na ile inayofuata dhidi ya Singida.
Alisema hatakuwa amewatendea haki Wanayanga endapo angeondoka na kurudi nyumbani wakati huu ambapo anabaki kupambana kuhakikisha timu yake inapata ushindi katika mechi hiyo.
"Nilipata taarifa za msiba huo dakika chache kabla ya kuingia uwanjani lakini sikutaka kumwambia mtu,unajua kule nyumbani mimi ni kama kichwa cha familia sasa kwa msiba wa aina yoyote natakiwa kushiriki kwa kiasi kikubwa,"alisema Lwandamina.
"Sitaweza kuondoka kwa namna yoyote na nimeshawaambia viongozi watulie nitawasiliana na ndugu zangu nafikiri watanielewa nataka kuhakikisha timu yangu inangia kwa nguvu Oktoba 28 ili tuweze kupata pointi tatu muhimu."