Kumbe Masoud Djuma chanzo Simba kupata pointi moja

Muktasari:

  • Wadau hao wanasema, Djuma ambae aliachwa Dar es Salaam kwa programu maalumu na baadhi ya wachezaji ni sababu ya Simba kupata matokeo hayo.
  • Hii ni kwa sababu, Aussems hana uzoefu na mikoa ya Tanzania na namna ambavyo wanazicheza mechi za namna hiyo.

 Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems alimwacha msaidizi wake, Masoud Djuma katika safari ya Mtwara walipocheza na Ndanda FC, lakini walichokutana nacho huko ni suluhu iliyowaibua wadau wengi wa soka.

Wadau hao wanasema, Djuma ambae aliachwa Dar es Salaam kwa programu maalumu na baadhi ya wachezaji ni sababu ya Simba kupata matokeo hayo.

Hii ni kwa sababu, Aussems hana uzoefu na mikoa ya Tanzania na namna ambavyo wanazicheza mechi za namna hiyo.

Mchambuzi makini wa soka, Ally Mayai amesema: “Djuma anazijua timu kuliko Aussems, lakini pia hata mechi za mikoani anazijua vizuri namna ya kuzicheza."

Amesema, Djuma ni muhimu kwenye timu kwa sababu aliweza kukaa mwenyewe katika benchi akiongoza Simba na kutengeneza mfumo wake wa 3-5-2, ambao ulifanikiwa na kuchukua ubingwa.

"Kukosekana kwake kwenye timu, inaweza ikawa sababu kubwa iliyochangia wakapata matokeo hayo yaliyowapa pointi moja,” alisisitiza Mayai mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.

Mayai aliongeza na kusema, Aussems pia, alikosea kutumia mfumo wa kuwacheza washambuliaji watatu wakati uwanja haukuwa rafiki kwake katika kufanya mashambulizi.