Chambua amvulia kofia Cannavaro

Muktasari:

Chambua aliyewahi kuwa kocha msaidizi Yanga alimpokea Cannavaro kipindi hicho akijiunga na timu hiyo akitokea visiwani Zanzibar.

Dar es Salaam. Kiungo  wa zamani  wa Yanga, Sekilojo Chambua amewataka wachezaji wa timu hiyo kufuata nyayo za nahodha wao aliyetundika daluga hivi karibuni, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Chambua aliyewahi kuwa kocha msaidizi Yanga alimpokea Cannavaro kipindi hicho akijiunga na timu hiyo akitokea visiwani Zanzibar.
“Cannavaro alivyotua Yanga alikuwa akifanya makosa mengi kwenye uchezaji wake ambao ulikuwa ni wakutumi nguvu nyingi bila ya akili lakini alikuwa mwepesi wa kujifunza na kufanyia kazi makosa yake.
“Naamini wapo wachezaji kwenye kikosi cha Yanga na kwingineko ambao wanatamani kupata mafanikio kama ya Cannavaro nadhani hilo linaweza kuwasaidia kwa sababu soka ni mchezo wa kujifunza kila siku,”alisema Chambua.
Hata hivyo, Chambua ameipongeza Yanga kwa kusema wamefanya maamuzi sahihi kwa kuamua kumpa nafasi ya uongozi, Nadir baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio makubwa.
Agosti 12, Yanga itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mawenzi Market ya Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kumuaga rasmi Cannavaro.
Kabla ya mchezo huo kutakuwa na burudani ya muziki kutoka kwa Mr Blue, Afande Sele, Lulu Diva, Juma Nature na Billnas huku Yanga Queens ikicheza na Morogoro Kombaini.