Panga la Mkongo 2 tu
Muktasari:
- Yanga kwa sasa ina nyota saba wa kigeni akiwamo kipa Youthe Rostand (Cameroon), Papy Kabamba Tshishimbi (DR Congo), Donald Ngoma na Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Mrundi Amissi Tambwe na Mzambia Obrey Chirwa. Pia beki Mkongo, Festo Kayembe naye aliorodheshwa katika usajili wa Yanga, lakini hajacheza mchezo hata mmoja na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera ameanza tathmini ya kikosi hicho ili kukisuka upya na amepanga kutembeza panga litakalobakisha mapro wa kigeni wawili au mmoja tu waliopo sasa. Inaelezwa kuwa, Zahera ameridhishwa na baadhi ya nyota wa timu hiyo, lakini anataka maboresho zaidi ya kusaka wakali wa kuipa timu mafanikio.
KESHO Jumatano ikifika saa 3:00 usiku, mashabiki wa Yanga watakuwa wamejua matokeo ya mchezo wa timu yao dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, ila huku nyuma kuna panga litashuka kwa mapro wa kigeni.
Yanga kwa sasa ina nyota saba wa kigeni akiwamo kipa Youthe Rostand (Cameroon), Papy Kabamba Tshishimbi (DR Congo), Donald Ngoma na Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Mrundi Amissi Tambwe na Mzambia Obrey Chirwa. Pia beki Mkongo, Festo Kayembe naye aliorodheshwa katika usajili wa Yanga, lakini hajacheza mchezo hata mmoja na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera ameanza tathmini ya kikosi hicho ili kukisuka upya na amepanga kutembeza panga litakalobakisha mapro wa kigeni wawili au mmoja tu waliopo sasa. Inaelezwa kuwa, Zahera ameridhishwa na baadhi ya nyota wa timu hiyo, lakini anataka maboresho zaidi ya kusaka wakali wa kuipa timu mafanikio.
Imeelezwa kuwa, kwa sasa mabosi wa Yanga wanasaka fedha ili kuweka mambo sawa klabuni hapo, pia fungu hilo litatumika kufanya usajili wa maana kulingana na ripoti ya kocha wao. Mwanaspoti linafahamu kuwa, Zahera ameshakabidhi orodha ya mahitaji ya awali anayotaka yafanyiwe kazi katika usajili, lakini ametaka ripoti kamili itoke baada ya mchezo wa kesho wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon.
Katika mpango huo, Yanga inataka kubakiza mastaa wa kigeni wawili au mmoja kutegemeana na fungu watakalopata na wanne wanaweza wasicheze mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Gor Mahia ya Kenya Julai 18.
Mbali na maproo hao, pia panga lingine kubwa zaidi litashuka kwa wachezaji wa ndani ambao, wataonekana hawana ushindani na kigezo cha kwanza ni ubora, nidhamu na idadi ya mechi walizocheza.
Wachezaji wapya ambao watasajiliwa watakumbana na wakati mgumu zaidi kwa mikataba yao kuwekwa vipengele vyenye kuleta tija kwa klabu ambapo, kila mchezaji atakapomaliza miezi sita mkataba wake utarudishwa mezani kupima ufanisi wake.
MSIKIE NYIKA
Mwanaspoti lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika ambaye licha ya kukiri kuwepo kwa vikao hivyo vya siri, alisema wanataka kuhakikisha Yanga ya msimu ujao inakuwa na moto. “Ni kweli tunajadiliana kuhusu kuboresha timu yetu kama uongozi, lakini kwa sasa tunasubiri kwanza ripoti ya mwisho ya kocha wetu ambayo tutaipata baada ya mchezo ujao dhidi ya Rayon,” alisema Nyika.
“Tutazungumza na kocha kuna tathimini yake ya awali ameitoa ambayo kama uongozi tunakubaliana naye kwa kuwa hata kocha aliyetangulia alikuwa anasisitiza hayo hayo sasa ametuambia tusubiri amalize kazi ndipo atatukabidhi jukumu la kufanya.
“Tunataka kurudisha ubora wa Yanga uliozoeleka kwa mashabiki na wanachama wetu ni lazima tupige akili za mbali, tunatafuta nguvu ya fedha kwanza na kama mambo kama yatakwenda sawa basi tutaifanyia maboresho makubwa timu, kwa sasa siwezi kukwambia ni maeneo gani tusubiri ripoti kamili, lakini tumejipanga kwelikweli,” alisema Nyika.