DPP ashikilia jalada la Malinzi

Muktasari:

  • Viongozi hao wa TFF wanakabiliwa na mashtaka 28, yakiwamo ya utakatishaji fedha

 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka na utetezi kwa kushirikiana zifanye juhudi za kutosha kufuatilia jalada la kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Jamal Malinzi na wenzake lililopo kwa  Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).

Jalada hilo lipo kwa DPP kwa zaidi ya muda wa siku 37.

Hakimu  Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri aliagiza hilo leo baada ya kusikiza hoja zilizowasilishwa mahakama ni hapo na mawakili wa upande wa Mashtaka na utetezi.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mwendesha Mashtaka wa Takukuru,Leonard Swai kudai kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Swai alidai kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo kwa DPP na kwamba aliongeza na uongozi wa Takukuru na kwamba wanalifuatilia. 

Hivyo aliomba ipangiwe tarehe nyingine ili waweze kujua wamefikia wapi.

Kutokana na hoja zilizowasilishwa na Swai, Wakili wa utetezi, Abraham Senguji adai kuwa kutokana na mgongano wa ofisi ya DPP na Takukuru wanaoumia ni wateja wao ambapo wameshtakiwa kwa makosa ambayo hayana dhamana.

Mahakama ipo kwa ajili ya kuangalia haki za upande wa Mashtaka na utetezi.

Senguji alieleza kuwa kama upande wa Mashtaka hauwezi kukamilisha upelelezi waiondoe kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha mwenendo wa makosa ya Jinai.

Alibainisha kuwa waiondoe hiyo kesi mahakama ni na kwamba pale watakapokamilisha upelelezi, wawarejeshe kesi iendelee.

Na kwamba kama upande wa Mashtaka umeshindwa kuendesha kesi hiyo aliomba mahakama iwaachie huru washtakiwa hao.

Baada ya Senguji kueleza hayo, Swai alidai kuwa anakubaliana na kifungu hicho cha 91(1) ambacho kinampa DPP mamlaka ya kuifuta kesi wakati wowote pale anapoona inafaa na hata kuirejesha pia.

Swai alieleza kuwa washtakiwa hao hawatatendewa haki kwa sababu wataachiwa huru na kukamatwa tena na kwamba kesi hiyo itaanza upya na utakuwa ni usumbufu kwa washtakiwa.

Alidai kuwa Takukuru wakimaliza uchunguzi ni lazima jalada liende kwa DPP alipitie na atoe maelekezo kama upelelezi uliofanywa unajenga kesi ama la.

Hata hivyo aliongeza kudai kuwa makosa ya kughushi yanahitaji utaalam katika kuyathibitisha na yanachukua muda mrefu katika uchunguzi.

Hivyo aliomba muda wa kufuatilia jalada hilo na kesi imeahirishwa hadi Novemba 30,2017.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga.

 Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 28, yakiwamo ya utakatishaji fedha wa Dola za Marekani, 375,418.