Yanga yawakimbia warembo Shelisheli

Muktasari:

Yanga ipo nchini humo kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya St Louis itakayochezwa Jumatano hii

Shelisheli. Yanga ipo katika mazingira salama kuelekea mchezo wao dhidi ya St. Louis, keshokutwa lakini maisha waliyokutana nayo hapa yamegeuka gumzo kwa msafara wake uliotua jana jioni.

Uongozi wa Yanga ni kama ulipiga bao la kisigino kwa kuiweka timu hiyo pembezoni mwa mji kwani ingekuwa kinyume huenda hali ya utulivu kwa wachezaji kuelekea mchezo huo ingekuwa ndogo.

Asilimia kubwa ya maeneo ya katikati ya Mji Mkuu wa Shelisheli, Victoria ambako Yanga imepakwepa imekuwa na sehemu nyingi za starehe hasa zikichagizwa na idadi kubwa ya watalii ambao wamekuwa wakimiminika visiwani humo kila wakati.

Tofauti na nyumbani ambako ni nadra kuona watu wakijazana kwenye kumbi za starehe katika kipindi ambacho sio mwisho wa wiki, kwa Shelisheli wao kila wakati wanautumia kufanya starehe.

Wakati suala la kujisitiri miili likipigiwa kelele kwa kiasi kikubwa nyumbani Tanzania,  Shelisheli ni kinyume kwani asilimia kubwa ya wakazi wake wamekuwa wakivaa nusu utupu.

Wanawake wa Shelisheli ambao ni warembo kimuonekano ndio vinara wa kuacha wazi miili yao hata wanavyokuwa kwenye shughuli zao za kawaida na linaonekana sio jambo la kushangaza kwao.

Ni vigumu kukutana na raia wa Sheliaheli akiwa amevaa mavazi yanayofunika mwili mzima tofauti na Tanzania ambako jamii yake inazingatia vilivyo maadili katika uvaaji.