Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rooney amchana Salah, ampa ushauri Slot

Muktasari:

  • Oktoba 4, 2025, Liverpool imepoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Chelsea kwenye Ligi Kuu England ikiwa ni kichapo chao cha tatu mfululizo katika michuano yote msimu huu. Matokeo hayo, yameifanya Arsenal kukaa kileleni mwa msimamo wa Premier baada ya kushinda 2-0 dhidi ya West Ham.

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney amemvaa nyota wa Liverpool, Mohamed Salah akisema mchango wake kwa sasa umekuwa mdogo wakati huu ambao timu hiyo inapitia kipindi kigumu.

Oktoba 4, 2025, Liverpool imepoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Chelsea kwenye Ligi Kuu England ikiwa ni kichapo chao cha tatu mfululizo katika michuano yote msimu huu. Matokeo hayo, yameifanya Arsenal kukaa kileleni mwa msimamo wa Premier baada ya kushinda 2-0 dhidi ya West Ham.

Salah, alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England msimu uliopita alipofunga mabao 29 wakati Liverpool ikitwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi kumi dhidi ya Arsenal iliyomaliza ya pili.

Hata hivyo, msimu huu amefunga bao moja pekee kutokana na mchezo wa wazi kwenye ligi, na Rooney amesema kwamba pale Salah anaposhindwa kuamua matokeo kwa mabao au pasi za mwisho, ndipo watu huanza kuangalia kwa makini zaidi nyanja nyingine za mchezo wake.

“Tunajua hafanyi kazi kubwa ya kurudi nyuma kujilinda, lakini katika mechi dhidi ya Chelsea, beki wake wa pembeni alikuwa akiteswa sana na yeye alikuwa anaangalia tu,” amesema nahodha huyo wa zamani wa England kupitia kipindi chake cha The Wayne Rooney Show, ambacho sasa kinapatikana kupitia BBC Sounds.

“Hakuwa anarudi nyuma kusaidia, na wachezaji kama [Virgil] Van Dijk na viongozi wa chumba cha kubadilishia nguo wanapaswa kumwambia, ‘unahitaji kusaidia wenzako.’

“Hilo lilikuwa jambo la kutia wasiwasi, na ninaona kama amepoteza mwelekeo kidogo wiki hii iliyopita.

“Wakati mambo yanaenda vizuri unapofunga mabao na kushinda mechi kila kitu kinaonekana kizuri na timu inavumilia hilo, lakini wiki hii iliyopita ningependa kuuliza kuhusu nidhamu yake ya kazi uwanjani.”

Salah alifunga bao la nne katika ushindi wa Liverpool wa mabao 4-2 dhidi ya Bournemouth kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu, huku bao lake lingine pekee la Ligi Kuu likiwa penalti ya dakika za mwisho dhidi ya Burnley.

Kutokana na ukweli kwamba Juni 2025 Salah alitimiza miaka 33, Rooney amependekeza abadilishwe nafasi kutoka kuwa mshambuliaji wa pembeni na kusimama kati kunaweza kumsaidia kurejea katika kiwango cha kutoa mchango mkubwa ambacho mashabiki wa Liverpool wamekizoea tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2017.

“Nadhani unapokuwa unazeeka kidogo, [Arne] Slot angeweza kuliona hilo na kufikiria, Chelsea wanatuharibu upande huu wa kulia,’ ameongeza Rooney, ambaye alishinda taji la ligi mara tano akiwa na Manchester United.

“Angeweza kumhamishia (Salah) katikati na kumuweka [Florian] Wirtz upande huo wa kulia, ili kubaki na nidhamu ya kazi uwanjani huku ukitumia ubora wa Salah kujaribu kufunga mabao. Kocha bora huona mambo kama haya na kufanya marekebisho. Sisemi kwamba amuache nje ya timu.

“Tulikuwa na hali kama hiyo kwa [Cristiano] Ronaldo kule Manchester United, naye pia hakuwa akirudi nyuma sana, kwa hiyo Ferguson (Sir Alex Ferguson) alimhamishia katikati. Hivyo, timu ilikuwa na uwiano mzuri wa kazi kufanyika, huku Ronaldo akiendelea kuwepo uwanjani kwa sababu alikuwa na uwezo wa kufunga na kuamua mechi.”