Oscar afunguka siri ya utajiri wake
Muktasari:
- Badala yake, kiungo huyo wa zamani wa Brazil amesema yeye na familia yake waliishi kwa kutumia bonasi za mechi, huku mishahara yote ikiwekwa kwenye akaunti maalumu bila kuguswa.
LONDON, ENGLAND: NYOTA wa zamani wa Chelsea, Oscar, amefichua siri ya mafanikio yake ya kifedha akisema siri yake hakuwahi kutumia hata senti moja ya mshahara wake mkubwa alipokuwa akiichezea Shanghai Port nchini China.
Badala yake, kiungo huyo wa zamani wa Brazil amesema yeye na familia yake waliishi kwa kutumia bonasi za mechi, huku mishahara yote ikiwekwa kwenye akaunti maalumu bila kuguswa.
"Nilikuwa naweka mshahara wangu wote kwenye akaunti tofauti na sikuwahi kuugusa hata mara moja. Mimi na familia yangu tuliishi kwa kutumia bonasi za mechi, ambazo nazo zilikuwa kubwa sana," amesema Oscar.
Oscar alitoa kauli hiyo alipokuwa mgeni katika podikasti ya The Obi One, inayoendeshwa na aliyekuwa kiungo mwenzake wa Chelsea, John Obi Mikel.
ALIUSHANGAZA ULIMWENGU
Mwaka 2017, akiwa na umri wa miaka 26 na bado akiwa kwenye kiwango kizuri, Oscar aliwashangaza wengi baada ya kuondoka Chelsea na kujiunga na Shanghai Port (wakati huo Shanghai SIPG).
Chelsea iliikubali ofa ya pauni 60 milioni, ambayo wakati huo ilikuwa rekodi ya mauzo ya klabu.
Ripoti mbalimbali zilidai kuwa Oscar alikuwa akilipwa zaidi ya pauni20 milioni kwa mwaka baada ya kodi, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa wachezaji waliolipwa zaidi duniani.
Ingawa imekuwa ikidaiwa alikusanya zaidi ya pauni150 milioni katika kipindi chake cha miaka saba nchini China, Oscar amesema kiwango hicho si sahihi, lakini hakukanusha kuwa alipata fedha nyingi.
MAFANIKIO CHINA
Katika kipindi chake Shanghai Port, Oscar alicheza mechi 248, akifunga mabao 77 na kutoa asisti 142.
Pia alisaidia klabu hiyo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya China pamoja na Kombe moja la FA la China.
Baada ya kuondoka China mwaka 2024, alirejea katika klabu yake ya utotoni ya Sao Paulo mwaka 2025 kabla ya kutangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 34.
ALING'ARA CHELSEA NA BRAZIL
Oscar alijiunga na Chelsea mwaka 2012 akitokea Internacional ya Brazil na kucheza mechi 203, akifunga mabao 38 na kutoa asisti 31.
Akiwa Stamford Bridge alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu England, Kombe la Ligi na Europa Ligi.
Katika timu ya taifa ya Brazil, alicheza mechi 48, akisaidia nchi yake kushinda Kombe la Mabara mwaka 2013, huku pia akitajwa katika kikosi bora cha Kombe la Dunia 2014.