Mashabiki wa Argentina, England wazomeana wakati wa nyimbo za taifa
Muktasari:
- Uwanja uliojaa mashabiki jijini Atlanta uligeuka kuwa uwanja wa vita vya sauti, huku mashabiki wa Argentina wakizomea kwa nguvu wimbo wa taifa wa England, “God Save the King,” kiasi cha kufanya usisikike vizuri.
ATLANTA, MAREKANI: KULIZUKA taharuki na hali ya uhasama kabla ya kuanza kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya Argentina na England, baada ya mashabiki wa pande zote kuzomeana wakati wa nyimbo za taifa.
Uwanja uliojaa mashabiki jijini Atlanta uligeuka kuwa uwanja wa vita vya sauti, huku mashabiki wa Argentina wakizomea kwa nguvu wimbo wa taifa wa England, “God Save the King,” kiasi cha kufanya usisikike vizuri.
Mashabiki wa England nao hawakukaa kimya, walijibu mapigo kwa kuzomea wimbo wa taifa wa Argentina, hali iliyoongeza joto kabla hata mpira haujaanza.
Wakati wachezaji wa timu zote walikuwa wakiimba nyimbo zao za taifa uwanjani, kelele za mashabiki zilifanya hata watazamaji waliokuwa wakifuatilia kupitia televisheni washindwe kuusikia vizuri muziki wa nyimbo hizo.
Baadhi ya mashabiki wa England walionyesha kutoridhishwa na kitendo cha wapinzani wao kuzomea wimbo wa taifa.
Mmoja aliandika kwenye mitandao ya kijamii:”Mashabiki wa Argentina hawajaonyesha heshima kwa wimbo wa taifa wa England. Twende England!”
Mwingine amesema:”Mashabiki wa Argentina walikuwa na kelele sana kiasi kwamba huwezi hata kuusikia wimbo wa England.”
Wapo pia waliotaja kitendo hicho kuwa cha kukatisha tamaa. Lakini mashabiki wa England nao walihakikisha hawabaki nyuma. Kabla hata wimbo wa taifa wa Argentina haujaanza kupigwa, tayari walikuwa wameanza kuzomea kwa sauti kubwa kama njia ya kulipiza kisasi.
Aidha, baadhi ya mashabiki wa Argentina walionekana wakiimba nyimbo za kuwakejeli Waingereza wakati wa wimbo wa taifa wa wapinzani wao.