Josko Gvardiol: Messi, Salah, Haaland sio watu wa kawaida
Muktasari:
- Gvardiol, mwenye umri wa miaka 23, anachukuliwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa kizazi cha sasa, kutokana na kiwango chake kizuri akiwa ni raia wa Croatia.
Beki wa Manchester City, Josko Gvardiol, ametaja majina matatu ya wachezaji wagumu zaidi aliowahi kukabiliana nao uwanjani akiwemo Lionel Messi, Mohamed Salah, na Erling Haaland.
Gvardiol, mwenye umri wa miaka 23, anachukuliwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa kizazi cha sasa, kutokana na kiwango chake kizuri akiwa ni raia wa Croatia.
Uchezaji wake mzuri kwenye fainali za Kombe la Dunia la FIFA 2022 uliifanya Manchester City kuvunja benki na kumsajili akitokea RB Leipzig ya Ujerumani, kwa Pauni 90 milioni majira ya joto mwaka 2023.
Katika mahojiano na ESPN UK, Gvardiol ametakiwa kuwataja wachezaji watatu wagumu zaidi aliowahi kuwakaba. Bila kusita, alimtaja Lionel Messi kama mchezaji wa kwanza.
Gvardiol amewahi kukutana na Lionel Messi mara mbili katika historia yake ya soka la ushindani, ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2021-2022; RB Leipzig ikifungwa 3-2 dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwaka 2022 wakati wa fainali za Kombe la Dunia, ambapo Argentina iliishinda Croatia mabao 3-0 kwenye mchezo wa nusu fainali, Messi alifunga kwa penalti. Hata hivyo, Gvardiol aliwahi kumtaja Lionel Messi kama mfano wake wa kuigwa
Mchezaji wa pili kwenye orodha yake ni Mohamed Salah, ambaye amekutana naye mara moja tu, wakati Manchester City ikipoteza dhidi ya Liverpool msimu uliopita.
Wa tatu ni Erling Haaland, ambaye kwa sasa ni mchezaji mwenzake wa Manchester City, tayari wamekutana mara tatu kabla ya kuwa pamoja.
Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2021-2022 akicheza RB Leipzig ambayo iliishinda Borussia Dortmund kwenye mchezo wa Ligi ya Ujerumani mabao 4-1.
Msimu wa 2022-23 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester City ikiiondosha Leipzig kwa jumla ya mabao 8-1 kwenye hatua ya 16 bora.
Gvardiol ameshaitumikia Manchester City katika mechi 103, akifunga mabao 11 na kutoa pasi za mabao 7. Msimu wa 2024-2025, beki huyo alifunga mabao 2 katika mechi 3.
Alipoulizwa kuhusu kiwango chake cha kufunga mabao, aliweka wazi kuwa Messi ni mchezaji anayemvutia zaidi, akifichua kuwa alipokuwa mdogo alicheza nafasi nyingi tofauti uwanjani.
Akihojiwa na Sky Sports, Gvardiol amesema: "Mchezaji wangu wa kuigwa ni Messi. Ukiwa beki kwa miaka 10-15, unachoka!"
"Nilipokuwa mdogo nilicheza kila sehemu uwanjani, mshambuliaji, winga, kiungo wa ulinzi, na hata kiungo wa mashambulizi. Najisikia huru popote ninapocheza. Mara nyingi najikuta nikicheza upande wa kushoto kwa sababu ndivyo kocha anavyotaka."
Wakati huohuo, Lionel Messi, akiwa na umri wa miaka 38, bado anaendelea kung’ara. Akiwa na Inter Miami, tayari ameisaidia timu hiyo kwa kuchangia mabao 32 na asisti 17 katika mechi 41 msimu huu kwenye mashindano mbalimbali.