Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Robert Matano: Ligi ya Tanzania unachoka kabla ya mechi

Muktasari:

  • Juni 27, 2025, KCB ilitambulisha Matano kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Soka Kenya ambayo ipo raundi ya nne.

UNAMKUMBUKA Kocha Robert Matano aliyeinoa Fountain Gate msimu uliopita? Sasa baada ya kuachana na timu hiyo amerejea nyumbani kwao Kenya na kutua KCB huku matumaini yakiwa ni kuipa taji la kwanza la ligi timu hiyo.

Juni 27, 2025, KCB ilitambulisha Matano kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Soka Kenya ambayo ipo raundi ya nne.

KCB inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 18, baada ya kucheza mechi nne na kukusanya pointi sita.

Matano ambaye maarufu kwa jina la Simba, amefanya mahojiano maalum akiwa Kenya na kuzungumzia mambo mengi yanayomuhusu kwenye safari yake ya ufundishaji huku akiwa na kumbukumbu ya kushinda mataji ikiwemo Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati sasa Kombe la Kagame mwaka 1984 alipoiongoza AFC Leopards kuichapa Gor Mahia.

Katika mahojiano hayo, Matano amesema amepata nguvu mpya ya kuendeleza urithi wake katika soka la Kenya baada ya kutua KCB.

“Sitabadilisha njia yangu ya kufanya kazi kwa sababu ya kizazi kipya cha Gen Z. Hata wao wanataka kushinda, na wanaojua wanataka kushinda tayari wanajua kinachohitajika,” amesema.

Anajieleza kama kocha anayejibadilisha kulingana na mchezo na anasema KCB imempa sapoti kubwa katika kazi yake.

Kuhusu madai ya kutumia uchawi kushinda mechi, Matano alijibu kwa kejeli: “Ikiwa uchawi unashinda mechi, basi watu wangesajili waganga wacheze.”

Kisha akaongeza kwa tabasamu: “Soka ndiyo kitu pekee ninachokifahamu maishani. Labda kingine ni kucheza muziki wa Rhumba, ambao hunipa furaha sawa na kushinda mechi.”

Mbali na hilo, Matano ametoa uzoefu wake wa kufanya kazi na timu ya Ligi Kuu Tanzania, huku akibainisha hakupendezwa na hali aliyoikuta.

“Wachezaji wengi wa Kitanzania hawajitumi vya kutosha. Ni vigumu kuwapata kwenye kiwango kizuri hasa wakicheza dhidi ya Simba au Yanga. Zaidi ya hayo, safari za ligi kule ni ndefu sana, unachoka kabla ya mechi,” amesema.

Historia inaonyesha Februari 26, 1984, Robert Matano aliketi kwenye basi la timu ya AFC Leopards majira ya saa 12 jioni, ilikuwa ni muda wa timu kuondoka Uwanja wa Nyayo kuelekea kambini Jacaranda Hotel, eneo la Westlands jijini Nairobi.

Leopards ilikuwa imetoka kuifunga Gor Mahia kwa mabao 2-1 kwenye fainali ya michuano ya Cecafa mwaka huo, na dereva wao, baada ya kuweka gari kwenye gia ya “neutral”, naye akawa miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya basi hilo.

Katika shamrashamra za ushindi, mashabiki wa Ingwe waliamua kulisukuma basi hilo hadi hotelini ikiwa ni umbali wa takribani kilomita sita uliomalizwa kwa muda wa saa tatu. Matano alishuka kwenye basi hilo akiwa na somo la maisha ambalo halitamsahaulika.

“Wakati huo nilijifunza maana halisi ya ushindi kwa mashabiki. Tangu siku hiyo nilitamani kuwa mshindi kila wakati ili nirudie hisia zile na kuwapa wengine furaha kama ile,” Matano ameiambia Nation Sport katika Kituo cha Michezo cha KCB, Ruaraka, wiki iliyopita.

Kituo hicho, kinachojulikana kama “The Den” kwenye duru za michezo nchini Kenya, ni nyumbani kwa Matano akiwa na dhamira ya kuirudisha furaha ya ushindi kwa timu ya KCB.

KCB, ambayo inajivunia timu tishio za rugby kwa wanaume na volleyball kwa wanawake, haijawahi kuwa na mafanikio makubwa kwenye soka. Katika kipindi cha miaka 32 tangu kuanzishwa, klabu hiyo imeshinda makombe mawili pekee ambayo ni Transparency Cup (sasa FKF Cup) mwaka 2003 na Nairobi Provincial League mwaka 1996.

Baada ya timu mpya kama Kenya Police FC na Nairobi United kushinda FKF Premier League na FKF Cup msimu uliopita, uongozi wa KCB ulishtuka na kuamua kubadilisha mwelekeo, ukitaka kuona timu yao ikipanda daraja la juu la ushindani. Ndipo wakaamua kumteua Robert Matano kuwa kocha mkuu, uamuzi ulioashiria dhamira kubwa ya klabu hiyo.

Matano amekuwa akifundisha soka kwa zaidi ya miaka 40 katika klabu takribani 17, kuanzia Pumwani Sportiff mwaka 1986. Ameonyesha uwezo wa ushindi kila alipoenda. Amezipandisha timu saba hadi Ligi Kuu na kushinda FKF Cup akiwa na World Hope (2005) na AFC Leopards (2017).

Pia, ameshinda ubingwa Ligi ya Kenya akiwa na Sofapaka mwaka 2009 na Tusker FC mwaka 2012 na 2021. Alishinda tena mwaka 2022, lakini FKF chini ya Nick Mwendwa ilifuta msimu huo uliosimamiwa na Caretaker Committee ya serikali.

“Ushindi na kudumisha utamaduni wa ushindi vinahitaji nguvu nyingi na ubunifu,” amesema Matano huku akiuelezea ushindi wa Sofapaka mwaka 2009 kama mfano bora wa mapambano yaliyofanikiwa.

Sofapaka, ikimilikiwa na mfanyabiashara wa Kongo, Elly Kalekwa, ilivuruga soka la Kenya mwishoni mwa miaka ya 2000 kwa kutumia mbinu za kipekee. Watu walidhani timu hiyo ilikuwa na pesa nyingi, lakini Matano amefichua ukweli.

“Watu walidhani tunalipwa vizuri sana, lakini hatukuwa na fedha nyingi. Nilitumia muda mwingi kuzungumza na wachezaji ili kuwahamasisha kuliko kufundisha. Wakati mwingine, ushindi ni zaidi ya mbinu, ni hali ya kiakili,” amesema.

Mwaka 2012, mbinu zake za ukocha ndizo zilizoleta tofauti alipoiwezesha Tusker kutetea taji lao. Aliteuliwa baada ya klabu hiyo kuachana na Sammy ‘Pamzo’ Omollo akiwa amesalia na mechi 10. Matano aliiongoza Tusker kubadilisha matokeo na kushinda ligi kwa kishindo kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Nairobi City Stars, wakishinda 3-0 katika uwanja wa Hope Centre. Tusker iliipiku Gor Mahia, iliyokuwa mbele kwa pointi moja kabla ya mechi ya mwisho.

“Nilikuwa nashindana na makocha ambao hawajawahi kushinda ligi. Nilijua siwezi kushindwa nao,” amesema kwa majivuno.

Siku hiyo, Matano alionyesha ukali wake kwa nidhamu. Alimwacha benchi kipa wa kwanza Boniface Oluoch kwa kuchelewa kufika uwanjani, na kumwanzisha George Opiyo.

“Nidhamu na bidii ni msingi wa mafanikio yangu. Nilipoteza wazazi nikiwa mdogo na nililelewa kwenye nyumba tofauti tofauti. Nilihitaji kuishi kwa nidhamu ili niweze kuendelea. Wanaoniona mkali, huo ndiyo ukweli wa maisha yangu,” amesema Matano.

Alizaliwa Mombasa mwaka 1965, ingawa alidanganya kuwa alizaliwa mwaka 1964 ili aweze kuanza kufanya kazi mapema. Jina lake lilitokana na mwanasiasa Robert Stanley Matano, rafiki wa baba yake.

Anapoulizwa kuhusu familia yake, anasema ana wake watatu lakini anakataa kutaja idadi ya watoto. “Wanaume wa Kiluhya hawahesabu watoto,” amesema kwa utani.

Akiizungumzia Tusker (2018–2024), Matano alieleza wazi hasira zake kwa uongozi wa klabu hiyo.

“Walitaka nishindwe. Hawakuniletea wachezaji niliowaomba. Nilifanya kazi kwa mazingira magumu, lakini bado nilishinda mataji mawili na sikuwahi kumaliza chini ya nafasi ya pili,” amesema.

Anampongeza sana aliyekuwa mwenyekiti wa Tusker, James Musyoki, pamoja na viongozi wengine kama Ambrose Rachier, Dan Mule, Elly Kalekwa, na Lt. Gen. Juma Mwinyikai, akisema walikuwa viongozi waliowaamini makocha.

Matano anakumbuka pia msaada alioupata kutoka Ulinzi Stars wakati alipougua figo, akiwashukuru sana kwa kumsaidia kupata matibabu.

Matano alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Austin Oduor, nahodha wa zamani wa Gor Mahia, na pia aliwahi kuishi na Jonathan Niva, aliyemfundisha nidhamu na kumtabiria kuwa atakuwa kocha.

Licha ya mafanikio yake yote, hajawahi kupewa nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.

“Wanaotoa ajira huko wanajua sababu zao. Mimi siombi kazi,” amesema kwa msisitizo.