Vituko na vimbwanga vya kusisimua AFCON
Muktasari:
- Kila mashindano hayo yanapofanyika baada ya miaka miwili kabla ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hivi karibuni kutangaza kubadilisha na sasa kuanzia 2029 yatafanyika kila baada ya miaka minne, kuna mambo yanayoibuka na kuacha alama katika historia ya michezo ya fainali hizo.
FAINALI za Kombe la Mataifa la Afrika (Afcon) 2025 zinazoendelea Morocco ni za 35 tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo 1957 na zimekuwa na matukio mengi ya kihistoria ya kuvutia, kusikitisha na pia kushangaza.
Kila mashindano hayo yanapofanyika baada ya miaka miwili kabla ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hivi karibuni kutangaza kubadilisha na sasa kuanzia 2029 yatafanyika kila baada ya miaka minne, kuna mambo yanayoibuka na kuacha alama katika historia ya michezo ya fainali hizo.
Nilibahatika kuyaona baadhi nilipohudhuria tatu kama mwandishi wa michezo wa magazeti ya serikali ya Daily News kwenye nchi tofauti kuanzia miaka ya mwisho ya 1960 hadi mwanzoni mwa 1980.
Leo ningependa kuodhoresha baadhi ya matukio ambayo yakizungumziwa historia ya fainali za Afcon sio haki kutoyaorodhesha.
CAF iliamua 1965 kuruhusu wachezaji si zaidi ya wawili wanaocheza nje ya nchi zao kuwemo katika vikosi vinavyowakilisha nchi zilizoingia fainali.
Hii ilitokana na Ghana iliposhiriki kwa mara ya kwanza 1963 na kubeba kombe wachezaji wake wote isipokuwa wawili walitoka Ulaya ambao walikuwa wanachezea klabu mbalimbali. Ghana ilibeba ubingwa kwa kuifunga Sudan 3-0 kwenye mchezo wa fainali.
Sheria hiyo ilitmika mpaka 1982 ilipofutwa na ndio maana leo baadhi ya nchi huwa na wachezaji si zaidi ya sita ambao wanachezea klabu za nchi zao.
Machi 1974 nilikuwa Cairo na mwandishi maarufu Sekione Kitojo aliyekuwa anafanya kazi na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kuandika habari za fainali za Afcon. Nilishuhudia mengi ambayo sitayasahau, lakini nitagusia mawili ambayo naona ni ya historia.
Kwanza ni Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) kuzuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo shehena yao ya nyani zaidi ya 50 waliofika nayo kama chakula cha wachezaji.
Hii ilizua patashika na ni baada ya mjadala wa viongozi wakuu wa nchi hizi mbili, Mobutu Sese Seko ( aliyekuwa rais wa Zaire) na Anwar Saadat wa Misri ndipo Wakongomani waliokwenda na wapishi wao waliruhusiwa kuondoka na nyani waliokwenda nao katika ofisi yao ya ubalozi na huko ndiko walipikiwa chakula.
Jingine ni mchezo wa fainali uliorudiwa kati ya Zaire na Zambia. Kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 hadi zilipomalizika dakika 30 za nyongeza na ukafanyika mchezo wa marudiano baada ya siku mbili na Zaire kushinda 2-0.
Mabao yote manne ya Zaire katika hizo mechi mbili yalifungwa na Mulamba Ndaye ambaye alifunga jumla ya mabao 9 katika fainali hizo. Mulamba baadaye alikuwa na maisha magumu Zaire, na alioona serikali ilikuwa haijali mchango wake katika kandanda alihamia Afrika Kusini na aliiaga dunia Januri 2019 akiwa na miaka 70.
Lipo pia suala la Cameroon iliyokuwa haishikiki fainali hizo 1980 na 1990, na kikosi chake cha kina Roger Milla, Thomas N'Kono, Joseph-Antoine Bell, Emmanuel Kunde, Stephen Tataw na François Omam-Biyik kilipata umarufu mkubwa kila pembe ya dunia. Kikosi hicho kilibeba kombe 1984 na 1988 na kufungwa na Misri katika fainali 1986.
Vilevile kuna hili la Zambia. Mnamo Aprili 27, 1993 ndege iliyochukua timu ya Zambia kwenda Gabon kwa hatua za mwisho za kukata tiketi ya fainali za Afcon iliangukia katika Bahari ya Atlantiki na kuua watu 30 wakiwemo wachezaji 18.
Ukiachana na hayo, lipo pia tukio la watu wanane waliofariki dunia na zaidi ya 40 kujeruhiwa katika vurugu nje ya Uwanja wa Yaounde, Cameroon waliokuwa wanataka kuingia kuangalia mchezo kati ya Cameroon na Comoro wakati wa fainali za Januari, 2022.
Ukiachana na hilo, basi la kikosi cha Togo liliwahi kushambuliwa na waasi waliokuwa wanapambana na majeshi ya Angola mara baada ya kuvuka mpaka wa Kongo na kuingia Cabinda (Angola), Januari 8, 2010.
Timu hiyo ilikwenda Angola kushiriki hatua ya mwisho ya kusaka tiketi ya fainali za Afcon. Togo ilijitoa katika mashindano na ikashangaza kuona CAF ikiipiga marufuku isishiriki mashindano mawili na kuitoza faini ya Dola 500,000.
Hatua hiyo ililaaniwa na nchi kadhaa za Afrika kama kitendo kilichokosa utu na thamani ya maisha.
Mbali na hilo, kuna jambo la Ivory Coast iliyofanya maajabu ilipokuwa mwenyeji wa fainali za 2023, ambapo awali iliboronga katika michezo ya makundi na kuonekana kuwa moja ya timu dhaifu katika mashindano. Hata hivyo, ilifanikiwa kutinga mzunguko wa pili kupitia wastani bora wa alama na nafasi katika kundi.
Awali katika makundi nchi hiyo iliifunga Guinea Bissau mabao 2-0, ikafungwa 1-0 kisha ikachapwa 4-0 na Equatorial Guinea. Lakini, baada ya hapo ikawa haishikiki na kufika fainali ambako ilikutana na Nigeria na kwa mshangao wa wengi ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Baada ya mechi za makundi na kufanikiwa kusonga mbele ilimtimua kocha Jean-Louis Gasset na nafasi yake kuchukuliwa na Emerse Fae ambaye alikuwa hana uzoefu wa kuongoza timu katika mashindano makubwa.
Mashabiki wa Ivory Coast waliunga mkono kufukuzwa kwa Gasset, lakini walipinga uteuzi wa Fae wakiuelezea kuwa uliiacha 'mbovu' nam kumchukua 'aliyeoza'.
Lakini, Fae alionyesha maajabu na kuiwezesha Ivory Coast hatimaye kubeba kombe. Mara baada ya kutimuliwa wakati mashindano yakiendelea Gasset alirudi kwao Ufaransa akilalamika kwamba wachezaji walimuangusha.
Gasset aliichezea Montpeliier kwa miaka 10 kabla hajawa kocha wa Caen na Isters za Ufaransa na kuwa kocha msaidizi wa PSG ya Ufaransa na Espanyol ya Hispania.
Baadaye alikuwa kocha wa Montpellier 2016–17 na kumaliza nafasi ya 15, hatua moja tu juu ya mstari wa timu zilizoteremka daraja. Aliporejea Montpellier 2024-25 timu ilishika mkia na kuteremka daraja na huo ukawa mwisho wa safari yake ya ukocha wa soka.
Casset alikusudia kwenda Morocco baada ya kupata mwaliko wa kuhudhuria fainali zinazoendelea za Afcon, lakini siku chache kabla ya kuanza mashindano alipata matatizo ya afya. Aliaga dunia Ijumaa iliyopita, Desemba 26, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 72 na anatarajiwa kuzikwa Jumapili ijayo.
Sasa tunasubiri fainali zinazoendelea Morocco zitakuwa na matukio gani yatakayoacha alama katika historia ya mashindano hayo makubwa kabisa ya kandanda ya Bara la Afrika.