Vita Kundi F AFCON 2025, haijaisha hadi iishe!
Muktasari:
Ivory Coast ipo kileleni kwa baada ya kukusanya pointi nne katika mechi mbili, sawa na ilivyo kwa Cameroon yenye pointi nne pia.
RABAT, MOROCCO: MSIMAMO unavyosoma kwenye Kundi F la mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 umenoga kwelikweli na timu zote nne zipo kwenye mchakato wa kuwania kukamatia tiketi ya kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora.
Ivory Coast ipo kileleni kwa baada ya kukusanya pointi nne katika mechi mbili, sawa na ilivyo kwa Cameroon yenye pointi nne pia.
Kisha inafuatia Msumbiji yenye pointi tatu na Gabon inaburuza mkia ikiwa haina pointi yoyote baada ya kuchapwa kwenye mechi zote mbili zilizochezwa katika mashindano hayo ya Afcon 2025 yanayoendelea huko Morocco.
Utamu unakuja sehemu moja tu, hata Gabon ambayo haina pointi, endapo kama itashinda mechi yake ya mwisho kwenye makundi, itakusanya pointi tatu, ambazo zitawaweka kwenye harakati za kusaka mtoano. Gabon itashuka uwanjani Stade de Marrakech kukipiga na Ivory Coast, ambao ni mabingwa watetezi wa mikikimikiki hiyo ya Afcon.
Balaa la mechi hiyo ni kwamba, Ivory Coast inahitaji ushindi ili kuongoza kundi, lakini pia ikiogopa kuwa kwenye hatari ya kukutana na kigogo kwenye hatua ya 16 bora katika mtoano wa mashindano hayo.
Kasheshe jingine katika kundi hilo litawahusisha Msumbiji na Cameroon. Miamba hiyo itakipiga uwanjani Stade Adrar na kwamba kila timu itahitaji ushindi ili kuingia mtoano kwa kishindo na kutishia wapinzani wao.
Ushindi kwa Msumbiji utawafanya kufikisha pointi saba na utaiacha Cameroon na pointi zao nne na ndiyo maana mechi hiyo inatabiriwa kwenda kuwa na ushindani mkali muda wote uwanjani, kila mtu akipigania nafasi yake. Patachimbika.
Mechi nyingine za kukamilisha hatua ya makundi zitakazopigwa Jumatano ni za Kundi E, wakati Equatorial Guinea itakapokuwa na kazi nzito ya kuwakabili Algeria uwanjani Moulay Hassan na Sudan kukipiga na Burkina Faso huko Stade Mohamed V.
Kwenye kundi hilo, Algeria tayari imeshafuzu hatua ya mtoano baada ya kukusanya pointi sita katika mechi mbili na bila ya shaka itawapumzisha wachezaji wake nyota akiwamo Riyad Mahrez na kwamba itakabiliana na Equatorial Guinea, ambayo haina pointi yoyote.
Sare yoyote kwa Algeria itawafanya kufikisha pointi saba na hivyo kuongoza kundi hilo. Hii itakuwa mechi ya kawaida tu, yenye hadhi ya kukamilisha kundi mengine yaendelee.
Shughuli pevu itakuwa kwenye mechi ya Sudan na Burkina Faso. Hawa watauana, kutokana na kila mmoja kukusanya pointi tatu, hivyo ushindi kwa kila timu ni muhimu ili kufikisha pointi sita.
Mambo ni moto. Sudan ilionyesha mchezo mzuri dhidi ya Equatorial Guinea, hivyo itahitaji kushuka uwanjani kwa moto uleule kuwakabili Burkina Faso. Itakuwaje? Ngoja tuone maana kwenye makundi hayo, vita haijaisha hadi kuisha kabisa.