Hakimi freshi, yupo tayari kwa AFCON 2025
Muktasari:
- Hakimi alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwenye tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwezi uliopita, lakini alionekana kwenye hafla hiyo mjini Rabat akiwa anatumia magongo, hali iliyozua mashaka kama angepona kwa wakati.
MCHEZAJI Bora wa Afrika na nyota wa Morocco, Achraf Hakimi, amesema amepona jeraha la kifundo cha mguu na yuko tayari kucheza katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inayoanza leo Jumapili.
Hakimi ametoa taarifa hiyo leo Jumamosi katika mkutano na waandishi wa habari,a ambapo ushiriki wa nahodha wa Morocco katika mashindano hayo yanayofanyika nyumbani ulikuwa mashakani baada ya kuumia mishipa ya kifundo cha mguu alipokuwa akiichezea Paris Saint-Germain (PSG) dhidi ya Bayern Munich katika Ligi ya Mabingwa mwezi uliopita.
Tangu wakati huo, kumekuwa na tetesi nyingi kuhusu hali yake ya kupona, lakini Hakimi mwenye umri wa miaka 27 alikuwa na hali ya kujiamini siku moja kabla ya mechi ya ufunguzi dhidi ya Comoros.
Morocco ambao ndio wenyeji wa mashindano itavaana na Comoros mjini Rabat, ingawa bado haijulikani kama Hakimi atapewa muda zaidi wa kupumzika kabla ya kucheza.
“Ninajisikia vizuri. Ninafuata mpango wa matibabu na madaktari pamoja na kocha (Walid Regragui). Baada ya hapo, tutaona kocha ataamua nini. Unaweza kumuuliza yeye,” amesema Hakimi na kuongeza;
“Niliogopa baada ya kuumia. Sikupenda kukosa Kombe hili la Mataifa ambalo tunaliandaa nyumbani. Nilitaka kuwa pamoja na timu. Sijui nitaanza kucheza lini, lakini ninajisikia niko tayari."
Kocha Walid Regragui amemshukuru beki huyo kwa juhudi kubwa alizofanya wakati wa kupona.
“Alifanya zaidi ya ilivyotarajiwa,” amesema kocha huyo kwenye mkutano huo wa waandishi wa habari na kuongeza;
“Jeraha lake halikuwa rahisi. Alifanya maamuzi magumu kwa ajili ya nchi yake. Kama kocha na kama Mmorocco, nataka kumshukuru hadharani. Ni mfano wa kuigwa.”
Hata hivyo, Regragui hakuthibitisha kama Hakimi atacheza katika mechi ya kwanza ya Kundi A ya leo Jumapili.
“Je, aanze au tumpe mapumziko? Tutaona, hilo ni uamuzi wangu,” amesema kocha na kuongeza;
“Anaweza kuanza leo… au asianze.”
Hakimi alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwenye tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwezi uliopita, lakini alionekana kwenye hafla hiyo mjini Rabat akiwa anatumia magongo, hali iliyozua mashaka kama angepona kwa wakati.
Hata hivyo, alitajwa kwenye kikosi mapema mwezi huu na baadaye akaonekana akifanya mazoezi pamoja na wachezaji wengine wiki hii.