Man United ‘yamshusha’ Andrey Santos
Muktasari:
- Santos, mwenye umri wa miaka 22, ametia saini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Old Trafford hadi mwaka 2031, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
MANCHESTER, ENGLAND: KLABU ya Manchester United imekamilisha usajili wa kiungo wa Brazil, Andrey Santos, kutoka Chelsea kwa dau la pauni 50 milioni.
Santos, mwenye umri wa miaka 22, ametia saini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Old Trafford hadi mwaka 2031, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Kiungo huyo amesema ni ndoto kutimiza kuchezea United, akieleza kuwa atajifunza mengi chini ya kocha Michael Carrick.
Mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo, Jason Wilcox, amesema Santos alikuwa mmoja wa malengo makuu ya usajili kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza maeneo mbalimbali ya kiungo.
Usajili huo unakuja wakati United ikiendelea na mazungumzo ya kumleta Youri Tielemans kutoka Aston Villa baada ya kuachana na mpango wa kumsajili Ederson wa Atalanta.
Staa huyo wa zamani wa Santos ya Brazil akiwa na Chelsea alifanikiwa kucheza michezo 47 na kufunga mabao 3 akiwa anatajwa kama mchezaji anayeaminika kuwa anaweza kuwika zaidi miaka miwili au mitatu baadaye.
United imefanya usajili huu ili kuhakikisha kuwa inakuwa na kikosi bora msimu ujao wa ligi ambao malengo ya timu hiyo ni kuhakikisha kuwa inaanza kurejea makombe makubwa likiwemo lile la Ligi Kuu England ambalo msimu uliopita lilichukuliwa na Arsenal kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22.