'Slot anaikosea sana Liverpool, atakuja kujuta'
Muktasari:
- Wakati akichambua mechi hiyo iliyopigwa nchini Uturuki kupitia kituo cha ESPN, Burley amekosoa mwenendo wa Slot wa kutumia wachezaji ambao hawako kwenye nafasi zao sahihi.
GWIJI wa soka nchini Scotland, Craig William Burley ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu uamuzi wa kiufundi wa kocha wa Liverpool, Arne Slot, baada ya timu hiyo kupoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa bao 1-0 dhidi ya Galatasaray jana Jumanne, Septemba 30, 2025.
Wakati akichambua mechi hiyo iliyopigwa nchini Uturuki kupitia kituo cha ESPN, Burley amekosoa mwenendo wa Slot wa kutumia wachezaji ambao hawako kwenye nafasi zao sahihi.
Amesema uchaguzi huo unavuruga mwenendo wa kikosi cha Liverpool kuwa mzuri katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa msimu, tofauti na alivyofanya msimu uliopita.
"Inaonekana kuwa Arne Slot anajaribu kuingiza wachezaji kwenye nafasi zisizo na mfano wake ili kujifunza mambo," Burley amesema.
"Hebu angalia ana mchezaji kama Frimpong, una Bradley, lakini mara kadhaa umekuwa akimtumia Szoboszlai kama mlinzi wa kulia, lakini huyu ni kati ya viungo bora zaidi katika soka la Ulaya. Kwa sababu umenunua wachezaji fulani, kwa nini unaipa wakati mgumu timu kwa kulazimisha mambo yasiyowezekana, ili hali kuna wachezaji zaidi ya mmoja ambao unaweza kuwatumia?"
Wakati Burley akikosoa uamuzi wa Slot wa kumchezesha Dominik Szoboszlai kama mlinzi wa kulia, pia ametambua kuwa kiungo huyo raia wa Hungary alifanya vyema katika nafasi hiyo katika mechi alizochezeshwa. Hata hivyo, gwiji huyo anaamini anachokifanya kocha huyo ni matumizi mabaya ya kipaji cha mchezaji huyo.
"Hata ingawa amefanya vyema kidogo katika baadhi ya mechi kwa kumtumia kwenye nafasi ya beki wa kulia, lakini inanishangaza kwamba amefikia hatua ya kuweka wachezaji kwenye nafasi zisizo sahihi, hapa kuna haja na Slot kujitafakari kwa kina," amesema mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea.
Burley pia alionesha wasiwasi kuhusu suala la kiufundi katika sehemu ya kiungo ambalo kwa sasa linaikabili Liverpool baada ya usajili wa majira ya kiangazi. Amesema uamuzi wa Slot wa kutaka kuwatumia wachezaji wake wenye majina makubwa unavuruga mwelekeo wa kikosi chake.
"Kwa sababu ikiwa Szoboszlai atacheza, Gravenberch atacheza, na jana ilikuwa Jones, lakini kwa kawaida alikuwa Mac Allister, kama hawa wachezaji watatu lazima wacheze, basi Florian Wirtz hatacheza au anapaswa kuhamishwa nafasi, na ikiwa Wirtz atacheza kwenye namba kumi, basi kuna mchezaji anapaswa kuhamishwa nafasi, na hili linaifanya timu kuwa kwenye msukomsuko wa kupambana na kupoteza mwelekeo kwa siku zijazo," amesisitiza Burley.
Liverpool kwa sasa iko nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kucheza mechi mbili, ikishinda moja na kupoteza moja.