Slot ambwagia zigo la lawama Frimpong
Muktasari:
- Eddie Nketiah alifunga bao la ushindi katika dakika ya 97 kwenye Uwanja wa Selhurst Park, na kuiharibu rekodi ya Liverpool ambayo ilikuwa imeshinda mechi tano mfululizo za ligi kabla ya hapo.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot, amemwangushia zigo la lawama mchezaji wake Jeremie Frimpong kufuatia uzembe alioufanya ambao ulisababisha timu hiyo kupoteza kwa bao la dakika za majeruhi dhidi ya Crystal Palace na kuharibu rekodi yao ya kutopoteza mechi katika Ligi Kuu England tangu kuanza kwa msimu huu.
Eddie Nketiah alifunga bao la ushindi katika dakika ya 97 kwenye Uwanja wa Selhurst Park, na kuiharibu rekodi ya Liverpool ambayo ilikuwa imeshinda mechi tano mfululizo za ligi kabla ya hapo.
Palace ilijipatia bao la kwanza kupitia kwa Ismaila Sarr lililotokana na kona kabla ya Liverpool kusawazisha kwa bao jingine la dakika za jiooni la Federico Chiesa na mechi ilioneakana kuwa ingemalizika kwa sare.
Lakini Palace ikapata pointi zote tatu kupitia shambulizi lililoanza kwa mpira wa kurushwa ambapo wachezaji wa Liverpool walishindwa kuondoa mpira uliorudishwa kwa kichwa na Will Hughes. Nketiah aliuchukua vyema mpira huo kabla ya kuachia shuti kali lililoingia wavuni.
Slot alieleza kwamba Frimpong, aliyeingia katika dk74 kuchukua nafasi ya Ibrahima Konate, aliondoka katika eneo lake na kumwachia Nketiah nafasi ya kufunga.
“Leo inatakiwa tujilaumu sisi wenyewe kwa jinsi tulivyocheza. Mchezaji mmoja alitoka katika nafasi yake kwa sababu alitaka kushambulia kwa kushtukiza kwenda lango la wapinzani, jambo ambalo halikuwa na maana kwa wakati ule kwani muda ulikuwa umeisha, hivyo kilichohitajika ni kuzuia tu. Suala lililotugharimu sana leo. Ni mchezaji wetu mmoja alikuwa na mawazo ya kushambulia zaidi katika muda ule na matokeo yake akawapa wapinzani nafasi ya kufunga bao la ushindi na sisi tukapoteza mechi.
“Nawapa pongezi Palace, si mara ya kwanza tunapoteza kwao, hata kwenye Community Shield walitufunga. Walistahili kuongoza kwa mabao mawili au matatu katika kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili tulibadilika na tukatengeneza nafasi nyingi, jambo ambalo si rahisi kwenye uwanja huu.”