Prime
Pitso amkingia kifua Nabi Sauzi
Muktasari:
- Nabi aliachana na Yanga baada ya msimu kumalizika akiwa ameipata makombe matatu kwa msimu na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na taarifa zinasema ameshamalizana na Kaizer, hata hivyo inadaiwa ishu yake ya kutaka kwenda na wasaidizi imezua sintofahamu kwa sasa.
KOCHA mzoefu kwenye soka la Afrika, Pitso Mosimane, aliyesaini dili nono huko Saudia, amesema aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi anafaa kuifundisha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Nabi aliachana na Yanga baada ya msimu kumalizika akiwa ameipata makombe matatu kwa msimu na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na taarifa zinasema ameshamalizana na Kaizer, hata hivyo inadaiwa ishu yake ya kutaka kwenda na wasaidizi imezua sintofahamu kwa sasa.
Hata hivyo, Pitso aliyefundisha soka Afrika Kusini kwa muda mrefu na kuipa Mamelodi ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema anaamini Nabi atakuwa mtu sahihi kwenye kikosi cha Kaizer kwa kuwa ameshafanya vizuri akiwa na Yanga, akisisitiza kwa soka la kisasa Nabi kocha huyo anatakiwa kwenda na wasaidizi wake kwa kuwa wataifanya kazi yake kuwa rahisi.
“Nabi ni kocha mzuri, amechukua trebles mara mbili, nafikiri ameshafanya hivyo mara tatu lakini kwa miaka tofauti, ingawa miaka hii miwili amechukua mfululizo," alisema Pitso anayeinoa Al Wahda na kuongeza;
“Lakini soka la Tanzania siyo sawa na la hapa Afrika Kusini, kule kuna Yanga Simba, Azam na wengine, hakuna ambaye unaweza kumdharau. Nafikiri ni mtu ambaye anafahamu sana jinsi ya kupambana na presha na hilo amelidhibitisha baada ya kuifikisha Yanga kwenye fainali ya Shirikisho Afrika mwaka huu.
“Nafikiri anaweza kuipa mafanikio Kaizer, sina uhakika kwa kuwa sifahamu kuhusu viwango vya wachezaji wao, lakini kwa ishu ya kocha ni mtu sahihi.”
InaaminikaNabi na Chiefs wapo kwenye sehemu nzuri ya kukamilisha mkataba, lakini kipengele ambacho kinasumbua ni ishu ya Mtunisia huyo kwenda na wasaidizi wake wote na Pitso alisema ni jambo la muhimu kila kocha kuwa na watu wake.
“Hapana, sio jambo zuri kumtaka yeye bila wasaidizi wake. Unawezaje kufanya hivyo? Kwa levo ambayo yupo kwa sasa anatakiwa kuwa na timu yake ambao hawatakiwi kuuliza, wanafahamu unataka nini kwa muda gani," alisema Pitso na kuongeza;
“Hata mimi nina timu yangu ambayo nimekuja nayo hapa, sasa tumeiongeza zaidi tunaye kocha mpya wa makipa ambaye nilifanya naye kazi Al Ahli ya Saudi. Nimemchukua kwa sababu nyingi, anaongea Kiingereza vizuri, anaongea Kiarabu na pia nimeona anaweza kunisaidia.
“Anajua tamaduni zangu, anajua nataka timu icheze vipi, natengeneza timu kutoka nyuma kama ambavyo timu nyingi za Afrika Kusini zinafanya ndiyo maana sasa makipa bora ni bei ghali.
“Hivyo nami naunga mkono Nabi kutaka kwenda na watu wake kwa kuwa dunia ya sasa inataka hivyo,” alisema kocha huyo aliyetwaa Ligi ya Mabingwa pia akiwa na Al Ahly ya Misri.