Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man Utd haikujiandalia maisha baada ya Fergie

Muktasari:

Habari nyingi nzuri ni za siku zilizopita hadi kuondoka kwa kocha aliyepata heshima kubwa katika ulimwengu wa soka, Sir Alex Ferguson.

HABARI juu ya Manchester United ilivyokuwa, ilivyo sasa na matarajio ya baadaye ni nyingi sana hapa Uingereza, hasa England.

Habari nyingi nzuri ni za siku zilizopita hadi kuondoka kwa kocha aliyepata heshima kubwa katika ulimwengu wa soka, Sir Alex Ferguson.

Habari nyingi za sasa si nzuri, asilimia kubwa ni mbaya kwa klabu kwa maana ya wadau kuona mwenendo si mzuri japo United bado ipo nafasi za juu.

Nyingine zinazoandikwa magazetini hapa na kujadiliwa kwenye hizi tunazoita korido za soka ni tetesi zilizopitiliza. Kwamba kocha wa sasa atafutwa kazi na kuajiriwa orodha ya makocha!

Msingi ninaoweza kuujenga hapa ni kwamba Manchester United hawakufanya utafiti wa kutosha wala kujiandaa vya kufaa kwa ajili ya maisha baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka.

Hii imedhihirika baada ya aliyeajiriwa, David Moyes kuwa na udhaifu wa hali ya juu, lakini wakubwa wa Old Trafford walitakiwa wajue kwamba walikuwa wamemtwisha mwanadamu nyumba, angeibebaje? Haiwezekani.

Hata walipoona anaboronga hakuna kazi kubwa iliyofanywa kuhakikisha klabu inarudi kwenye reli na kwamba Old Trafford inarudi kuwa ngome isiyosogelewa au jeshi lisiloshindwa, ambalo kwake ni kawaida kutwaa mataji na fedheha kumaliza chini ya nafasi ya pili.

Kaajiriwa Louis van Gaal ambaye kwa miezi kadhaa sasa inaelezwa kibarua chake kipo matatani, japo nijuavyo mie kuna mtu akiamua aendelee, atafanya hivyo hadi mwisho, naye ni Ed Woodward.

Sipendi kuzungumzia sana mambo ya uwanjani na matokeo, kwani wengi wa wasomaji huyaona au kusoma; nijikite katika namna ya kuondoka kwa kocha huyo kulivyobadili mambo Manchester kuwa hasi kwenye maeneo kadhaa.

Van Gaal anakosa vionjo vilivyomfanya Fergie aheshimiwe hata na waandishi wa habari na kujenga umoja klabuni, si kama sasa yanaulizwa maswali kibao ya ajabu na Van Gaal anababaika, anakasirika au hata anatoroka chumba cha mahojiano.

Nakumbuka Ferguson, akitoka kwenye mazoezi, akipanda ngazi kwenda kwenye ile Media Centre iliyopo uwanja wao wa mazoezi wa Carrington kila Ijumaa, uliiona nguvu yake na ya klabu.

Ungeona waandishi walikuwa na wasiwasi, mawazo huku wakijaribu kujipanga jinsi watakavyopanga maswali yao kwa heshima na kuzingatia maadili asije akawazodoa.

Hakuna mwanahabari aliyechukulia kiutani mkutano na Fergie au na klabu yake, waliingia kwa adabu na kuondoka kwa adabu, mwenyewe akionesha ni nani hasa. Hakuna utani.

Fergie alihakikisha anadhibiti klabu na alianza mkutano wake kwa kufanya uchambuzi yakinifu wa mechi inayofuata, wapinzani wao walivyo ndipo maswali yakaanza.

Akiona tu mwandishi alikuwa dhaifu katika kujenga hoja, usahihi wa takwimu au jinsi ya kuuliza swali, alimtazama mhusika kama simba anayekaribia kumla, au daktari anavyomfanyia uchunguzi mgonjwa.

Kulikuwa kuna kitu kinaitwa ‘Mstari wa Fergie’, ambapo waandishi hawakutakiwa wala kutarajiwa kuuvuka katika maswali na majenzi ya hoja zao. Ukivuka, basi ungekuwa na uhakika ungepigiwa simu na Ofisa Habari anayeheshimika sana klabuni hapo, Karen Shotbolt kukuambia siku zako za kuripoti kutoka Carrington zimekwisha. Na hiyo ni kwa maelekezo ya Fergie.

“Habari hazitoki hovyo hovyo Manchester United,” ungemsikia Ferguson akijigamba mbele ya wasaidizi wake wakati wanahabari wakiondoka.

Hata kama haikuwa sahihi kwa asilimia 100, wale waliokuwa wamepangwa kuchukua habari klabuni kila siku, wanaweza kuthibitisha kwamba ilikuwa ngumu kupata stori kubwa kutoka kwa Fergie.

Lakini chini ya uongozi wa Van Gaal, klabu imegeuka kuwa ndoo inayovuja, kukiwapo watu wengi wanaojinasibu na United wakikubali kutoa maelezo juu ya mambo yanayoendelea klabuni kwa wanahabari, kila mmoja walau kwa dakika tano.

Kulikoni? Kwa sababu klabu hawakujiandaa na maisha baada ya mkongwe yule. Na yakishavuja, ndipo wakuu wanashituka na kujiuliza; hivi Fergie angefanyaje katika hali hii? Wanakuwa wameshachelewa! Hugundua kosa wakishatenda na hawazuii mengine kutokea.

Kuna vitu vingine ungeweza kuviona au kuhisi ni vidogo, lakini vilisaidia sana kujenga umoja klabuni na morali kwa wachezaji.

Ferguson alikuwa na mazoea ya kuwaita kwa heshima wafanyakazi iwe Old Trafford au Carrington, tena kwa majina yao ya kwanza, akawasalimu kila siku; “Habari za asubuhi …za mchana … za jioni?”

Na ujue hao ni pamoja na wafanyakazi wa ngazi za chini kama wasichana na kina mama wapika chai, jamaa wanaohangaika kuweka uwanja sawa, wafuaji nguo na wengine wengi.

Huleta maana kubwa sana na kuwafanya waanze siku vyema wanapotambuliwa na kocha wa moja ya klabu kubwa zaidi duniani na mambo yakawa yanaenda vyema klabuni na hata majumbani mwao.

Van Gaal ni tofauti sana, anataka wafanyakazi ndio wamheshimu, akipita waogope na kumwamkia anapopita kama mfalme kwenye korido za Carrington au Old Trafford. Hakuna mwanga wala joto ndani yake, kaganda tu.

Ferguson alikuwa akiitwa ‘meneja’ na wakati wote klabuni alihakikisha anafanya udhibiti vilivyo wa klabu na hakuruhusu mtu kumzunguka na kila mchezaji aliungwa mkono na Fergie; kama ni kumwonya alifanya wakiwa wawili.

Yamebadilika mengi, hakuna tena udhibiti tangu kuondoka kwa Ferguson, kaka yake aliyekuwa pia skauti mkuu Martin na Ofisa Mtendaji Mkuu David Gill.

Leo hii, Van Gaal anawabwatukia wachezaji wake hadharani, hutokea mgawanyiko kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na imefika mahali Ed Woodward anamzunguka na kuwaita wachezaji waandamizi kumjadili kocha. Mara wachezaji wanamwita kocha na kumwambia mfumo wake mbovu, ratiba yake haifai na kadhalika, kisha kocha ananywea! Hiyo haingetokea chini ya Fergie na ilijenga ‘afya’ klabuni na ikawa ngome kweli kweli.

Leo hii kocha anaulizwa kila aina ya swali naye anajibu kiajabu na kutengeneza stori vichekesho hivyo klabu kuonekana ya kitoto. Fergie nyakati fulani alikasirika, lakini alilenga kulinda watu na klabu yake.

Van Gaal anaelekea kwenye ‘point of no return’ nadhani, maana amefika mahali anaulizwa swali anakimbia chumba cha mahojiano akiwa mwekundu usoni.

Kocha huyu mwenye umri wa miaka 64 amefika mahali pa kumwita mwandishi wa Sun, Neil Custis ‘fat man’. Lugha hiyo inampotezea heshima na urafiki na haikupata kutokea kwa kocha Manchester United. Ikiwa anataka watu wamuunge mkono afanye jambo moja tu, Man U ishinde mechi zao.