Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cheki aibu hii ya Michezo ya Olimpiki kwa Tanzania

Muktasari:

Wakati tuliposikiliza rufaa zilizozihusu klabu hizi walikuwapo wajumbe ambao mjadala ulipoanza tu, bila ya kuambiwa na mtu, walitoka wenyewe nje ya ukumbi kwa sababu ni wapenzi wa moja ya klabu hizi.

KILA nikitafakari masuala ya michezo, hasa nilipokuwa mwandishi wa matukio mbalimbali, yapo mambo nikiyakumbuka huwa ninacheka peke yangu.

Hatimaye hujiambia ninakubaliana na usemi wa wahenga wa “kinyesi cha kale hakinuki”, lakini ukweli ni kwamba aliyekiona hapo zamani kila akiikumbuka harufu yake hujisikia karaha.

Mbali ya kuandika habari za michezo baada ya kucheza michezo mingi utotoni mwangu, ikiwa ni pamoja na gofu, kriketi, mpira wa magongo na tenisi, nilitumikia taasisi nyingi za michezo za nchini na za kanda.

Leo nitagusia moja ya matukio ambayo sitayasahau katika utumishi wangu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kipindi cha karibu miaka minane na hatimaye kujiuzulu baada ya kuona uamuzi wetu kila mara unawekewa mkwara na Wizara ya Michezo.

Wakati nikiwa mjumbe wa BMT nilishiriki kusikiliza rufaa, nyingi zikiwa za Yanga au Simba na hasa zilizohusu mvutano wa klabu hizi mbili maarufu za Dar es Salaam.

Wakati tuliposikiliza rufaa zilizozihusu klabu hizi walikuwapo wajumbe ambao mjadala ulipoanza tu, bila ya kuambiwa na mtu, walitoka wenyewe nje ya ukumbi kwa sababu ni wapenzi wa moja ya klabu hizi.

Walifanya hivyo kwa kuona haikuwa jambo la busara kushiriki katika kufikia uamuzi kutokana na kuwa na maslahi.

Mmoja wao aliyekataa kutia lake Simba ilipoguswa ni Dk. Wilbard Sarungi, wakati ule akiwa mkuu wa Hospitali ya Muhimbili na baadaye kuwa waziri.

Alikuwa akisema yeye ni Simba damu kama ile aliyoichezea hospitali alipokuwa akifanya upasuaji. Miongoni mwa mijadala ambayo siishau kutokana na hasira iliyozuka ni ule wa kukwama timu ya Olimpiki ya Tanzania kule Tokyo, Japani, ilipokuwa njiani kwenda Seoul, Korea ya Kusini, kushiriki michezo ya Olimpiki ya 1988.

Ni hadithi ya kusikitisha na iliyoitia aibu Tanzania katika michezo na ulimwengu wa kimichezo. Mengi tuliyoelezewa yalikuwa sio tabu kuyaamini na unaweza kusema hayaingii akilini.

Tuliarifiwa kuwa timu yetu iliondoka Dar es Salaam bila ya fedha na ilipofika Tokyo haikuweza kununua chakula wala chai kwa wanamichezo,

Katika sakata hilo wanamichezo wetu walikwama uwanja wa ndege kwa vile hawakuweza kulipiwa yaliyotakiwa uwanja wa ndege ili waweze kuendelea na safari ya kwenda Korea.

Lakini hatimaye wake na watoto wa mabalozi wa nchi za Kiafrika waliokuwapo Tokyo walilazimika kuchangishana fedha kuwapatia wanamichezo wetu chakula na kulipia huduma nyingine na kuweza kuendelea na safari .

Wanamichezo wetu walifika Korea wakiwa wamechoka hoi bin taabani na waliovunjika moyo kwa usumbufu walioupata katika safari yao.

Timu iliporudi nyumbani ilianza kazi ya kutafuta kilichosababisha kikosi chetu kukwama Tokyo. Wanariadha walisimulia kwa uchungu na wengine kulia juu ya namna walivyokaa na njaa muda mrefu uwanja wa ndege na wengine kuomba chakula.

Hapa nataka kukumbusha kuwa wakati ule ilikuwa sio rahisi kwa Watanzania kumiliki fedha za kigeni na ilikuwa kosa la jinai kumiliki hata Dola moja ya Kimarekani au Pauni ya Kiingereza bila ya kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Kilichobainika katika uchunguzi ni viongozi wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) waliokwenda na timu hiyo kwenye michezo walifanya uzembe.

Wao walisafiri kwa ndege nyingine na kupitia Ulaya na sio Japani kwa safari ya Korea na hiyo ndiyo sababu ya wanamichezo wetu kutopata fedha.

Baada ya kupata maelezo wajumbe wa BMT tulikubaliana wahusika wawajibishwe kwa kufukuzwa uongozi au kujiuzulu ili TOC ipate viongozi wataojali maslahi ya wanamichezo na heshima ya nchi.

Kilichotushangaza wajumbe ni ule utaratibu wa siku zile wa watu wanaojuana kulindana na kuoneana haya na kuweka mbele muhali bila ya kujali maisha ya watu na maslahi ya nchi.

Baadhi yetu tulikutana na Waziri aliyekuwa akishughulikia michezo, Fatma Said Ali na Katibu Mkuu wake, Tibakweitira. Tulibishana na kutoafikiana.

Nilimtegemea waziri niliyefahamiana naye tokea tukiwa wadogo Zanzibar angekuwa tayari kuwaudhi wachache wasiojali kuwaudhi Watanzania wengi kuliko kuwafurahisha wao na kulaumiwa na jamii.

Mimi na wenzangu tulimwambia waziri sisi katika BMT tulikuwa tayari kusamehe mengine na sio lile kwa sababu tuliamini Watanzania wasingetuelewa .

Tulimkumbuhsa Waziri Amina kwamba Daudi Mwakawago alituchagua wakati akiongoza wizara hiyo alisisitiza umuhimu wa kuweka maslahi ya Watanzania mbele kuliko urafiki na mtu au kikundi cha watu wachache.

Lililotushangaza ni kutakiwa tupunguze ghadhabu na tuwasamehe viongozi wa TOC.

Baada ya kuona uamuzi wetu haukukubaliwa na Wizara kwa sababu ambazo mpaka leo zinanishangaza wajumbe wengi, tukiongozwa na Mwenyekiti wetu, mwana taaluma mahiri wa habari Hamza Kasongo tulijiuzulu.

Wapo wajumbe waliotuunga mkono, lakini kwa vile walikuwa watumishi wa serikali hawakuweza kujiuzulu kutokana na mtumishi wa serikali hakuwa na haki ya kutafautiana na wakubwa, hata wakifanya maovu.

Walikuwepo wajumbe walioona mantiki ya kutaka iongozi wa TOC wawajibishwe, lakini waliona wangepoteza heshima ya kuwa viongozi wa BMT na kuamua kubana kimya wasipoteze nadaraka.

Mjumbe mmoja bila ya aibu alinifuata na kunionya ati tulikuwa unajitafutia balaa. Nilimwambia historia itatukumbuka na naamini Watanzania wa wakati ule na wa leo wataona tulifanya uamuzi sahihi.

Mvutano wetu na wizara ulisababisha BMT kuvunjwa na kwa bahati nzuri haikuelezwa kuwa ilikuwa “kwa maslahi ya umma”, kisingizio kilichotumika siku zile kuficha maovu.

BMT iliundwa upya na baadhi yetu tulioitwa wakorofi ikawa mwisho wa kulitumikia Baraza, lakini mpaka leo sijilaumu kwa uamuzi wangu kwa vile niliona haukuwa na dosari.

Tukio lile la kufumbia macho uoza lilinihakikishia imani niliyokuwa nayo kwamba mwenendo wa serikali wa kuvumilia uovu ndio uliopelekea TOC kwa muda mrefu kuwa kama mali ya watu fulani na sababu ya kuzorota michezo katika medani ya kimataifa.

Ninaamini ipo siku watafiti watalichungulia suala hili na kuieleza jamii ili makosa ya kulindana kwa maovu yasirejewe.

Nimeyaeleza haya sio kumuaibisha mtu bali kuonyesha namna baadhi ya viongozi wa michezo nchini zamani walivyojiamini kufanya watakavyo kwa kujua wangelindwa na wakubwa.

Kashfa ile ni sehemu ya historia, lakini natumai jamii haitakuwa tena tayari kuvumilia viongozi wa michezo wanaofanya jeuri bila ya kujali maslahi na heshima ya nchi.

Mungu ibariki Tanzania na watu wake.