Diamond uso kwa uso na Snoop Dogg

Unaweza kusema ni hasira za kukosa tuzo za ‘Bet Award’ au tamaa za  mafanikio, hiyo ni baada ya msanii Diamond Platnumz kuonekana kwenye picha mbalimbali akiwa studio na msanii staa kutoka Marekani ‘Snoop Dogg’.

Picha hizo ni muendelezo wa ziara ya msanii huyo nchini humo katika kutafuta wasanii tofauti ambao pengine huenda akafanya nao kazi kwa lengo la kuendelea kuutangaza muziki huo kimataifa na kumalizia albamu yake.

Diamond alianza ziara hiyo baada ya kushindwa kutwaa tuzo za ‘Bet Award’ ambayo ilienda kwa msanii kutoka Nigeria Burna Boy katika kipengele kilichokuwa na wasanii watano akiwemo Wiz Kid.

Hii sio mara ya kwanza mkali huyo wa kibao cha kamata kuonekana na masta hao wa muziki nchini Marekani, kwani siku kadhaa zilizopita, alionekana akiwa kwenye picha na mkongwe wa Hiphop, Busta Rhyems na baada ya muda mfupi alionekana pia na mkali wa michano Wiz Khalifa.

Ukweli anao Diamond mwenyewe juu ya kuonana na wasanii hao kama kuna taarifa njema za uwepo wa ‘collabo’ au ameamua kujitanua na mastaa hao kwa lengo la kuongeza umaarufu wake.

Mpaka sasa Diamond ameimba nyimbo tatu na wasanii tofauti kutoka Marekani akiwemo Neyo katika wimbo wa Marry You, Rick Ross wimbo wa Waka Waka na wimbo wa African Beauty aliomshirikisha Omarion.