SportPesa yaijaza tena Simba
KAMPUNI ya SportPesa ambao ni wadhamini wakuu wa Simba, leo wanatarajia kuijaza noti klabu hiyo kwa kuipa bonasi ya Sh 100 milioni kwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mkwanja watakaokabidhiwa jijini Dar es Salaam.
SportPesa pia ni wadhamini wakuu wa Yanga wakiipiga tafu pia Namungo na wanatarajia kukabidhi fedha hizo kwenye mchezo dhidi ya Namungo utakaotumika pia kwao kupewa kombe lao la Ligi Kuu Bara, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar, Amos Makalla,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Tarimba Abbas alisema watakabidhi hundi ya Sh100 milioni ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba walioingia na Simba.
Aliongeza kuwa hundi hiyo wataikabidhi Simba mara baada ya mchezo dhidi ya Namungo watakapokuwa wanajiandaa kukabidhiwa pia kombe lao.
“Huu ni msimu wa nne mfululizo kwa SportPesa kuwapa bonasi ya Sh100 milioni Simba baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu. Kama wadhamini tunatarajia kuwakabidhi hundi ya Sh100 milioni Simba baada ya kuchukua tena ubingwa msimu huu, hivyo tuwapongeze katika hilo,” alisema.
Tarimba aliongeza: “SportPesa tunaona fahari sana kwa jinsi Simba inatutoa kimasomaso, nembo ya kusportpesa kwa kupeleka mpira wa miguu kwenye ramani ya Afrika. Wanaitangaza SportPesa na ningewaomba wazidi kufanya vizuri zaidi kwani ni faraja kwetu.”