Singida yaizima Mtibwa ugenini
BAO pekee lililowekwa na straika Mkenya, Elvis Rupia dakika ya 44 lilitosha kuipa Singida Big Stars ushindi wa kwanza kwenye mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiizima Mtibwa Sugar iliyokuwa uwanja wa nyumbani wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Ushindi huo uliopatikana kwenye mechi iliyopigwa na kumalizika jioni ya leo Alhamisi, umeifanya Singida kufikisha jumla ya pointi tano ikitoka nafasi ya 12 hadi ya nane, huku ikizidi kuiweka pabaya Mtibwa ambao haijaonja ushindi ikiwa imesaliwa na pointi mbili ikiwa nafasi ya 14.
Katika mchezo huo, timu zote zilionyesha soka tamu, licha ya kuangushwa na uwanja, lakini ni wageni walioweza kutumia nafasi waliyoitengeneza kupata bao dakika moja kabla ya mapumziko kupitia Rupia aliyetua kikosini hivi karibuni kutoka Polisi FC ya Kenya.
Hilo lilikuwa bao la kwanza kwa mchezaji huyo aliyekuwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu Kenya (FKL) kwa msimu uliopita kwa kufunga mabao 27 akivunja rekodi iliyodumu nchini humo kwa miaka 47 tangu Mourice Ochieng aliyekuwa nyota wa Gor Mahia kufunga mabao 26 msimu wa mwaka 1976.
Singida inajiandaa kurudi nyumbani mjini Singida kujiandaa na mchezo ujao wa ligi hiyo dhidi ya Simba utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Liti, wakati Mtibwa itasafiri hadi Mbeya kuvaana na Tanzania Prisons siku hiyo ambayo jioni hii imetoka kucharazwa mabao 3-1 na Simba katika Uwanja wa Sokoine.