Nabi atia neno usajili Yanga, kufunguka Agosti 31

Kocha wa Yanga, Nasredine Nabi amesema kwa kiasi kikubwa uongozi wa timu hiyo, umeifanyia kazi ripoti yake katika mapendekezo ya usajili kama vile ambavyo alikuwa anahitaji.

Nabi alisema awali mapendekezo yake ya kwanza alikuwa anataka beki mwingine wa kigeni na tayari kuna mmoja ambaye wameshamalizana nae ila bado kuja nchini tu na kutambulishwa.

Alisema baada ya hapo kuna maeneo mengine kama katika pamefanyiwa kazi kwa kuongezwa washambuliaji wawili, Fiston Mayele na Heritier Makambo ambao anaimani wataongeza makali ya nafasi hiyo.

“Ukiunganisha nguvu ya wale waliokuwepo msimu uliopita kama Yacouba Sogne mfungaji bora wa timu pamoja na Mayele, Makambo naimani kubwa tutakuwa na safu kali ya ushambuliaji yenye uwezo wa kufunga mabao mengi kuliko msimu huu,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tumeimarisha safu yetu ya ulinzi kwa kusajili mabeki wa pembeni ambao naimani nao watakuja kuongeza uimara katika kuzuia na kuifanya timu yetu kutofungika kwa urahisi.”

Katika hatua nyingine Nabi alisema atakuwa na nafasi nzuri na uwanja mpana zaidi kuzungumzia usajili wa timu msimu huu na ripoti yake kiujumla pale dirisha litakapofungwa Agosti 31.

Nabi alisema bado kuna wachezaji wengine kama si watatu basi wawili ambao tutawasajili na baada ya hapo zoezi hili tutalifunga zaidi na wakati huo tutakuwa katika maandalizi rasmi ya msimu ujao.