Kisa Simba Bangala aingia chimbo, apewa dozi spesho

KISWAHILI cha kwenye Gahawa wanasema kaingia chimbo. Mkongomani Yanick Bangala hatacheza mechi dhidi ya Mbeya Kwanza Jumanne ijayo lakini Kocha wake, Nabi Mohammed amechekelea kwamba staa huyo kuanzia leo atakuwa na takribani siku 17 kabla ya kumvaa Mnyama Simba.

Nabi ameongeza kwamba hata kama asingekuwa na adhabu yoyote pengine asingemchezesha kwenye mechi hiyo akiwemo pia majeruhi Khalid Aucho ili kukusanya nguvu za mechi ya watani Desemba 11 ambayo ina heshima zaidi ya pointi.

Yanga imerudi kambini na kasi ya mazoezi makali ya mara mbili ndani na nje ya uwanja kuhakikisha wanalinda ubora wao.

Bangala amefikisha kadi tatu za njano tangu ligi ianze ambazo zitamzuia kucheza mchezo huo wa Jumanne ijayo mjini Mbeya lakini kocha wake anachekelea akisema hakuna shida chama limeenea.

Alionyeshwa kadi ya tatu katika mchezo dhidi ya Namungo na kocha Nesreddine Nabi ameliambia Mwanaspoti kwamba bado ana viungo wengi watakaoziba nafasi yake kwani kikosi cha msimu huu kimesukwa vizuri kila nafasi.

Kama haitoshi Nabi alisema amempa ruhusa Bangala kurejea kwao DR Congo kwa mambo yake binafsi na kwamba atatakiwa kurudi nchini haraka kabla ya timu hiyo kutoka Mbeya.

“Nikweli tutamkosa Bangala katika mechi ijayo bado tuna watu wa kuziba nafasi yake na tukacheza kwa ubora wetu,hiyo ni mechi ambayo tunahitaji ushindi kwa nguvu yetu,”alisema Nabi.

“Tutamkosa katika mecho hii dhidi ya Mbeya kwanza lakini tuna uhakika wa asilimia mia moja tutakuwa naye katika mchezo utakaofuata dhidi ya Simba ambao kocha yoyote angetamani kuwa na watu wake wote wa muhimu,”alisisitiza.

Alisema kukosekana kwa Bangala kunaweza kupozwa endapo Aucho atakuwa tayari katika mechi ijayo baada ya kukosa mechi iliyopita kutokana na majeruhi ya goti.

“Aucho anaweza kurejea ameanza mazoezi vizuri lakini bado tutamfuatilia maendeleo yake kama ataweza kuwa tayari kwa mchezo ujao au tuwe na mpango gani mpya,hayo yote tutayafanyia uamuzi kabla ya kuelekea Mbeya,”alisema Nabi ambaye msaidizi wake ni Cedrick Kaze raia wa Burundi.

Aucho na Bangala wamekuwa wakiipa thamani Yanga katika safu ya kiungo kwa ubora wao wa kupokonya mipira na kupiga za kupanga mashambulizi ya kupatikana mabao licha ya kwamba kikosi hicho msimu huu kimekuwa na mastaa wengi.

Yanga baada ya mechi na Mbeya Kwanza itapumzika kwa siku 10 kabla ya kuwavaa Simba.