GSM aweka Sh500 milioni mezani Yanga kuiua Simba
SIMBA wana tajiri wao Mohamed Dewji ‘MO’ lakini Yanga acha watambe na tajiri wao Ghalib Mohamed ‘GSM’ na sasa vinara hao wa Ligi Kuu Bara kama watashinda mechi hiyo watafunga msimu wakiwa watamu mfukoni usipime kwa mzigo ambao wamewekewa mezani.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba GSM ameamua kuongeza mzigo akiweka mezani Sh500 milioni kama wakiwatupa nje Simba katika mchezo huo wa leo wa nusu fainali ya Kombe la ASFC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa.
Alichofanya GSM ni kama kuongeza Sh 100 milioni zaidi katika ahadi ya awali ambayo aliiweka kwenye mchezo wa ligi lakini timu hizo zikaenda sare isiyo na mabao.
Inaelezwa kwamba katika salamu zake, bosi huyo amewatega wachezaji wake akiwaambia hawajawahi kumuangusha lakini mchezo huu anahitaji sana ushindi ambao utakwenda kuweka heshima kubwa kwao kama wachezaji.
Ahadi hiyo itaamsha mzuka kwa wachezaji wa Yanga kuelekea mchezo huo ambao safari hii ni lazima mshindi apatikane uwanjani ndani ya dakika 90 ama penalti.
“Tajiri ameshasema ameweka huo mzigo sasa kazi kwa vijana, unajua GSM anaipenda sana hii timu ukiacha suala la uwekezaji, hamjawahi kumuona anavyochanganyikiwa akiona Yanga haifanyi vizuri lakini kitu kizuri anawaamini sana wachezaji na anaamini watawafurahisha mashabiki,” kilisema chanzo.