Bao 5 zakatisha sikukuu FC Platinum
Muktasari:
KISHINDO cha mabao 5-0 Simba ilichoipa Majimaji kwenye Kombe la Shirikisho (FA) kimefika Zimbabwe kwa FC Platinum.
KISHINDO cha mabao 5-0 Simba ilichoipa Majimaji kwenye Kombe la Shirikisho (FA) kimefika Zimbabwe kwa FC Platinum.
Kocha wa Platinum, Norman Mapeza amekatisha sherehe za wachezaji na benchi lake na kurejea mazoezini jana asubuhi kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Simba.
Awali, kabla hajatangaza warejee mazoezini jana alikuwa ametoa angalizo kali kwamba hakuna starehe za kupitiliza na kila mmoja ajichunge asipate corona ambayo inaweza kusababisha kukosa safari ya Dar es Salaam timu ikaathirika. Ofisa Habari wa timu hiyo, Mwanamama, Chido Chizondo alisema jana kwamba; “Tunapata changamoto ya ratiba za ndege za Dar es Salaam ndiyo maana itatulazimu kusafiri siku ya mwaka mpya na tutaondoka kule Januari nane. Itatubidi kukaa Dar es Salaam wiki nzima.”
Kocha Mapeza amewaambia viongozi kuwa mechi ya Jumatano ijayo jijini Dar es Salaam ni ngumu kutokana na umuhimu wake, hivyo ni lazima waifanyie mazoezi ya kutosha kwani ushindi wa bao 1-0 walioupata hauwahakikishii usalama.
“Tunalazimika kuendelea na mazoezi kwa vile tuna mechi ngumu ya ugenini na muhimu sana kwetu, hasa ukizingatia wapinzani wetu huwa wanabadilika sana wanapokuwa kwao,” Mapeza alikiambia chombo kimoja cha habari mjini Harare.
Habari zinasema Platinum tayari wana video za mechi kadhaa za Simba ikiwemo ile dhidi ya Yanga na Simba jijini Dar es Salaam ambazo wanaamini ndizo zitawapa picha halisi ya mpinzani wao.
Kwa mujibu wa magazeti ya Zimbabwe, vigogo wa Platinum huenda wakatua Dar es Salaam kesho na hata kwenye mechi ya Simba na Ihefu watakuwepo.
Hiyo ndiyo itakuwa mechi ya mwisho ya Simba kabla ya kurejea kimataifa ambako wana dakika 90 tu za kutetea uhai wao na kufuzu hatua ya makundi.
Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck ametoa tamko kali akiwalinda na kuwatetea wachezaji wake dhidi ya wadau na mashabiki wanaodai kasi yao ya ushindi imeshuka.
Kocha huyo amewataka wamkosoe yeye na wachezaji wasiguswe.
“Watu wanaweza kulalamika kwamba timu yangu haijitumi, tangu Nigeria tunaumwa. Hakuna mchezaji ambaye hajaugua. Na wawe wanaumwa au hawaumwi wamekuwa wanajitoa.
“Nawataka watu waache kutukosoa, ongeleeni kuhusu mimi kwa kinachonihusu. Achaneni na wachezaji ambao wanajitoa kwa kila hali kwa klabu,” alisisitiza Sven kwa kufoka.
Kauli hiyo ya kocha imetokana na tathmini za wadau mbalimbali kwamba kiwango cha timu yake kimeshuka. Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Mlage Kabange anaamini kwamba wekundu hao wana nafasi kubwa ya kushangaza kama watajipanga, kujielewa na kucheza na hesabu. Winga wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema: “Wachezaji wanatakiwa wapambane sana ili kuendelea kuwa juu.”