Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nabi ashtuka...dirisha dogo Yanga inaleta kitu

KIKOSI cha Yanga kipo Lindi kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, huku benchi lake la ufundi chini ya Kocha Nasreddine Nabi likianza hesabu ya kufanya usajili kupitia dirisha dogo.

Yanga inataka kuwa na kikosi imara na kocha huyo ameshtukia kitu akitaka eneo moja la haraka kuboreshwa na anachofanya ni kuwaangalia kwanza mastaa wake waliopo na ikitokea ameshindwa ataingia sokoni haraka kuleta jembe jipya.

Kocha Nabi anapasua kichwa kupata mtu sahihi atakayekuwa na ubora wa kucheza kwa ufasaha katika wingi ya kushoto ambako amesema kuna tatizo na kunamvuruga kwa sasa.

Nabi alisema hesabu zake za kwanza ni kuendelea kumpa makali winga Farid Mussa ambaye amekuwa akitumika eneo hilo kwa baadhi ya mechi ili azibe nafasi ya Yacouba Songne atakayekuwa nje kwa muda mrefu kufuatia kufanyiwa upasuaji wa goti.

Yacouba amecheza mechi zote tano za msimu huu akitokea upande huo na kuifanya Yanga na kuwa na safu bora na yenye nguvu ya ushambuliaji kabla ya kuumia na kupelekwa Tunisia kufanyiwa upasuaji na jana asubuhi alirejea nchini kuendelea kujiuguza.

Nabi aliliambia Mwanaspoti kuwa, anataka mtu mwenye nguvu ya kuzalisha mashambulizi na kuwa tishio ambapo kama Farid akishindwa kazi tu ataingia sokoni kutafuta mtu bora zaidi.

“Kuna kazi kubwa ilikuwa inafanywa na Yacouba upande huu alikuwa akisaidia kuja kusumbua kukaba, pia alikuwa na nguvu ya kupandisha mashambulizi zaidi na kutengeneza mabao,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tuna Farid ni mchezaji mzuri, nitafurahi kama ataelewa ambacho nataka awe anakifanya sasa, nimeshakaa na kuzungumza naye ili awe na muendelezo mzuri wa kiwango chake.”

Kocha huyo ambaye kesho atakuwa na kibarua cha kuwakabili Namungo ugenini kusaka ushindi wa kwanza dhidi yao, alisisitiza kwa kusema;

“Tukishindwa kupata mtu wa kuziba nafasi hiyo itatulazimu tutafute mtu sahihi tunatakiwa kuwa na timu itakayokuwa na nguvu pande zote ili tuweze kufanya vizuri zaidi.”

Aidha kocha huyo aliyetua Jangwani mwaka jana siku chache baada ya kutemwa na Al Merrikh ya Sudan alikoifundisha kwa muda mfupi akimpokea aliyekuwa Kocha wa Simba, Didier Gomes, alisema katika mpango huo wa Farid pia ataangalia kumjaribu mshambuliaji wake mzawa pekee aliyemsajili msimu huu, Yusuf Athuman kama atakuwa na nguvu ya kuingia eneo hilo.

Yusuf alisajiliwa na Yanga akitokea Gwambina na bado hajaingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza, licha ya kutumiwa katika mechi kadhaa za ligi akiingizwa kipindi cha pili akitokea benchi.