Simba SC kuivaa Warundi Uwanja wa Lake Tangangika

Muktasari:

Simba SC inatumia michezo hiyo ya kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam utakaopigwa Oktoba 23 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC kesho Jumatano Oktoba 16, 2019 itacheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya Aigle Noir ya Burundi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Simba inakwenda katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata dhidi ya Mashujaa FC jana Jumatatu shukrani kwa goli bora lililofungwa na kiungo Sharaf Shiboub.

Simba inatumia michezo hiyo ya kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam utakaopigwa Oktoba 23 jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema michezo hiyo itawasaidi kuwaweka wacheza wao kuwa katika ushindani kila wakati na kuongeza ushindani wa namba katika kikosi chao.

Katika michezo yake ya kirafiki kocha wa Simba, Patrick Aussems ametoa nafasi kwa wachezaji wa kikosi cha vijana pamoja na wale wasiokuwa na namba katika kikosi cha kwanza kuonyesha uwezo wao.

Simba imekuwa na mwendelezo wa michezo ya kirafiki, kwani wiki iliyopita walianza na Bandari FC Uwanja wa Taifa na kuibuka na ushindi bao 1-0 lililofungwa na Ibrahimu Ajibu katika dakika ya 77 akipokea pasi ya Rashid Juma.