2025 haukuwa mwaka wa Simba

Muktasari:
- Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga, waliotwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.
LICHA ya kuonyesha kiwango bora Simba imemaliza msimu ikiwa mikono mitupu, bila kutwaa taji lolote katika mashindano yote iliyoshiriki jambo linalozua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga, waliotwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.
Hili linawaumiza zaidi mashabiki wa Msimbazi kwani Simba walionekana kuwa na kikosi kipana wakiamini huu ndio mwaka wao, kwani nyota waliosajiliwa walitarajiwa kufanya maajabu msimu huu.
Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho (TFF), Simba walijikuta wakiondolewa katika hatua ya nusu fainali, jambo ambalo halikutarajiwa kwa timu yenye historia kubwa na kiu ya mafanikio.
Matarajio ya mashabiki kuona Simba ikinyanyua kombe hilo yalikuwa makubwa kutokana na kiu yao ya misimu minne mfululizo ambayo walikuwa wanashuhudia ikienda kwa watani wao.

Kipigo kutoka kwa Yanga kwenye mechi ya mzunguko wa pili kiliwaumiza zaidi, si kwa sababu ya pointi tu ambapo Simba ilihitaji zote tatu, bali pia kwa sababu ya hadhi ya ‘Kariakoo Derby’. Kiwango kizuri kilichoonyeshwa na mastaa kama Elie Mpanzu, Jean Charles Ahoua na Kibu Dennis hakikutosha kuwazuia mastaa wa Yanga kama Pacome Zouzoua, Clement Mzize na wengineo kuitawala ligi.
Hiyo ni mitazamo ya baadhi ya mashabiki wa timu hiyo na soka kwa ujumla ambao furaha yao ni kuona timu inashinda na sio kufungwa lakini kwa takwimu Simba haikufanya vibaya zaidi ilionyesha kiwango bora.
Simba ilikosa utulivu na nidhamu ya matokeo kwenye mechi muhimu tu kwani Ligi Kuu kwenye mechi 30 ilishinda 25, sare tatu na kupoteza mbili zote dhidi ya Yanga.
Kwenye takwimu, Simba waliongoza kwa idadi ya mabao yaliyofungwa kwa mechi za ugenini lakini ilishindwa kulinda matokeo muhimu nyumbani.

Kiufupi Simba imecheza soka la kuvutia, imevunja rekodi za msimu uliopita iliomaliza katika nafasi ya tatu, lakini msimu umeisha bila taji na hilo linatosha kusema haukuwa mwaka wao.
Mwanaspoti imekuchambulia tathmini ya msimu mzima wa Simba ambao walikosa tu bahati ya kuchukua makombe lakini kwa takwimu walikuwa bora msimu huu.

KIKOSI KIPYA
Simba ilianza msimu kwa kusajili wachezaji zaidi ya 10 na kati ya hao wachezaji saba walianza kikosi cha kwanza ukimtoa Shomari Kapombe, Kibu Denis, Mohamed Hussein, Fabrice Ngoma ambaye ulikuwa msimu wake wa pili sawa na Che Malone na waliobaki walikuwa wageni.
Ikumbukwe wakati wachezaji hao wanatambulishwa Simba iliachana na nyota wao muhimu Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute, Luis Miquissone, Henock Inonga, Clatous Chama, John Bocco na wengine.
Mbali na wachezaji lakini walianza upya kulisuka benchi la ufundi wakamleta kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids na wenzie.
Kiufupi ni kwamba wekundu wa Msimbazi walianza upya kusuka kikosi hicho ambacho ndani ya muda mchache baadhi yao wamefanya vizuri akiwamo mfungaji bora, Charles Ahoua aliyemaliza na mabao 16, Lionel Ateba na Steven Mukwala waliomaliza na mabao 13.
Mbali na wafungaji pia kipa namba moja, Mousa Camara ulikuwa msimu wake wa kwanza kikosini hapo na alionyesha kiwango bora na kumaliza na clean sheet 19 mbele ya Djigui Diarra aliyekuwa nazo 17.

FAINALI
Mwanzoni mwa Msimu mipango ya Simba ilikuwa ni kufika nusu fainali ya michuano ya CAF na hiyo ni kutokana na kuishia robo kwa takribani misimu mitano.
Msimu huu Simba ilifika fainali na ilikuwa ya kwanza kwa timu hiyo katika michuano ya CAF tangu ilipocheza mara ya mwisho fainali ya Kombe la CAF Novemba 27, 1993 dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kulala 2-0.
Ukiangalia namna walivyozichanga karata zao hadi kufika fainali ni wazi ubora wa wachezaji ulifanikisha timu hiyo kuvuka malengo.
Fainali ilikutana na RS Berkane waliyowahi kukutana katika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Shirikisho msimu wa 2021-22.
Katika mechi hizo, Simba ilianza kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 kabla ya marudiano kupata sare ya 1-1 na ubingwa ukaenda kwa Berkane iliyoshinda jumla ya mabao 3-1.

AHOUA, CAMARA
Nyota hao wawili kwa kiasi kikubwa waliisaidia Simba kwenye michuano ya kimataifa na ile ya ndani.
Ndani ya msimu wa kwanza tu wamethibitisha kuwa ni wachezaji muhimu kikosini hapo kutokana na kile walichokionyesha.
Ahoua alikuja kipindi ambacho msimu wa nyuma aliyekuwa nyota wa Yanga, Aziz KI ndiye alikuwa mchezaji aliyeonyesha kiwango kikubwa na akafanikiwa kuchukua tuzo tatu, mfungaji bora, mchezaji bora wa msimu na kiungo bora.
Vivyo hivyo kwa Camara alisajiliwa wakati ambao alikuta upinzani kati ya Diarra na aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi.
Kwa takwimu, nyota hao wawili waliotokea Magharibi mwa Afrika wanaondoka na tuzo mbili kwa Camara kipa bora akimaliza na cleansheet nyingi na mfungaji bora ni Ahoua. Hao ni miongoni mwa wachezaji waliochangia kufanya bingwa wa Ligi Kuu asijulikane hadi siku ya mwisho. Licha ya kutobeba makombe, Simba imebadilika.