Prime
Kocha mpya Yanga kutua na straika

MEZANI kwa mabosi wa Yanga kwa sasa kuna majina mawili ya makocha wanaopigiwa hesabu, mmoja aje kuinoa timu hiyo kuziba nafasi ya Miloudi Hamdi aliyetua Ismailia ya Misri, lakini kuna jambo linaloweza kuwa na faida kwa klabu hiyo mara atakaposhuka kocha Mfaransa.
Hamdi aliyeipa Yanga mataji matatu ndani ya siku 148 alizokaa na timu hiyo tangu Februari 4 hadi Julai 2, amemaliza mkataba na ilipokuja ofa ya Wamisri hakutaka kuremba na kuufanya mchakato wa kuleta kocha mpya kurudi upya.
Kama ambavyo awali Mwanaspoti liliwajulisha kuwa kuna majina mawili yaliyokuwa yakipigiwa hesabu kuona mmoja anatua Jangwani, akiwamo Msauzi Rhulani Mokwena na Mfaransa Julien Chevalier, huku kocha huyo wa zamani wa Asec Mimosas ya Ivory Coast akipewa nafasi kubwa.
Mokwena aliyewahi kuzinoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Wydad Casablanca ya Morocco dau na ma- sharti yake yameonekana kuwa magumu, jambo linalotoa nafasi kubwa kwa Mfaransa kuja kuinoa timu hiyo, huku mpango wake wa kushuka na straika wa maana ukimpa ulaji zaidi.
Ipo hivi. Mokwena alishaweka wazi vitu anavyohitaji kama akija Yanga, lakini hatua ya Zamalek kumtaka kabla ya Waarabu hao kumchukua kocha mwingine ndio ilichelewesha makubaliano ya mwisho juu ya kocha huyo aliyeiwezesha Mamelodi kutwaa ubingwa wa African Football League.
Pembeni ya Mokwena, lipo jina la Julien Chevalier anayamalizia mkataba na ASEC ambaye naye kila kitu kimekamilika lakini anataka kitu kimoja tu.
Chevalier amewaambia Yanga kuwa, kama wanamtaka mshambuliaji Celestin Ecua Kuna njia atawapa ili wamnase kirahisi straika huyo ambaye ndiye MVP wa Ligi Kuu ya nchini humo iliyomalizika hivi karibuni ni yeye kutua Jangwani.
Yanga inamtaka Ecua ambaye ni mshambuliaji mwenye kasi na ujuzi wa kufunga aje kuungana na ndugu zake Pacome Zouzoua na Yao Akouasi anaotoka nao nchi moja, ili kuziba pengo la Mzambia Kennedy Musonda aliyemaliza mkataba na kuruhusiwa kuondoka klabuni hapo.
Hata hivyo, akili ambayo Yanga imepewa kuongea na klabu ya Zoman FC ambayo ndio iliyomtoa kwa mkopo kwenda Asec.
Yanga inataka kufanya maamuzi haraka ya kocha mkuu ili kuwahi maandalizi ya msimu mpya ikiwa ni pamoja na kumalizia usajili wa kikosi cha mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA), Kombe la Muungano na la Toyota.
“Kila kitu kipo sawa mambo yaliyosalia ni maamuzi ya mwisho tu ni yupi aje na kocha atakuja haraka sana ili tuwahi ratiba ya maandalizi,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga na kuongeza:
“Tunataka hatua za mwisho za usajili naye ashiriki kwa kuwa katika hao makocha waliobakia kila mmoja anaijua vizuri timu yetu kwa njia moja au nyingine.” Kwa namna ilivyo ni kwamba Mfaransa Chevalier ndiye ana nafasi kubwa ya kutangazwa kocha mkuu wa Yanga na atakapotua tu, klabu hiyo itakuwa na uhakika wa kumnasa Ecua ambaye katika msimu huu ameitumikia Asec mechi 24 za Ligi Kuu (Ligue 1) akifunga mabao 13 na kuasisti tisa.
Hata hivyo mchezaji huyo thamani yake inaelezwa ni Dola 250,000 (zaidi ya Sh 600 milioni) ana mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Zoman inayommiliki na alikuwa kwa mkopo Asec.